WATUMISHI WA NCAA WAPANDA MITI 1,000 NA MINGINE 10,000 WAGAIWA WANANCHI

Na Mwandishi wetu, Karatu - Watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) leo tarehe 28 machi, 2025 wameunga mkono kampeni ya upandaji miti iliyozinduliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda tarehe 15 machi, 2025 kwa lengo la kutunza mazingira na kuboresha mandhari ya mkoa wa Arusha ambao ni kitovu cha utalii hapa nchini. 

Akizungumza wakati wa zoezi la upandaji miti lilofanyika ofisi za NCAA Karatu, Afisa Uhifadhi Mkuu anayesimamia sehemu ya Usimamizi wa wanyamapori na utafiti Lohi Zakaria amesema lengo la zoezi la upandaji miti kwa watumishi ni kuunga mkono jitihada za serikali za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kutunza mazingira.
“NCAA leo tumetekeleza maagizo yaliyotolewa na mkuu wa Mkoa wa Arusha kupanda miti, siku ya leo pekee tumepanda miche ya miti 1,000, tunaungana na serikali kuhakikisha kuwa tunakabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi hasa swala la hewa ukaa ambalo dunia nzima kwa sasa linapambana nao” Alisema Lohi 

Kwa upande wake Afisa Uhifadhi Mkuu Dismas Macha, alieleza kuwa NCAA imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhamasisha wananchi wa vijiji vinavyozungukaa hifadhi kwa kuwagawia miche ya miti ambayo inazalishwa kutoka kwenye kitalu cha miti kinachotunzwa na NCAA ili wapande katika maeneo yao na kutunza uoto wa asili wa maeneo yanayozunguka eneo la hifadhi. 
Msimamizi wa kitalu cha miti NCAA Naman Naman amebainisha kuwa kuanzia tangu siku ya kilele cha maadhimisho ya siku ya upandaji miti duniani machi 21, 2025 hadi sasa, NCAA imegawa miche ya miti elfu kumi (10,000) kwa wananchi waliopo katika vijiji 17 vinavyopakana na Hifadhi ya Ngorongoro katika Wilaya za Karatu, Monduli na Meatu. 

Miche inayogawiwa kwa wananchi ina faida nyingi kwa jamii ambapo hutumika kama dawa, kupata mbao na kuni, matunda, kufugia nyuki, kuboresha mazingira na kuhifadhi ardhi

No comments