TFRA NA TAASISI ZA UTAFITI WA KILIMO ZAJADILI MASHIRIKIANO UDHIBITI WA MBOLEA
Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imekutana na kufanya mazungumzo na Taasisi za Utafiti wa kilimo zilizo chini ya Wizara ya Kilimo kwa lengo la kujadili ushirikiano baina yao katika masuala ya udhibiti wa mbolea hususani katika kufanya tafiti na majaribio ya mbolea zinazokusudiwa kusajiliwa nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa Mamlaka hiyo, Bi. Elizabeth Bolle, amesema kikao hicho kimelenga kujadili namna bora ya kufanya tafiti na majaribio ya mbolea ili ziweze kusajiliwa na kutumika nchini.
Kikao hicho kimefanyika jana tarehe 25 Machi, 2025 katika ukumbi wa TFRA, Kilimo IV-Temeke, jijini Dar es Salaam, ambapo maazimio na mapendekezo yenye lengo la kuimarisha udhibiti wa mbolea nchini na kuboresha ushirikiano baina ya TFRA na taasisi hizo yametolewa.
Bolle ameeleza kuwa, Ufanyaji wa tafiti/majaribio ya mbolea unalenga kuhakikisha kuwa mbolea zinazowafikia wakulima zinakuwa na ubora unaotakiwa ili kuleta tija inayokusudiwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Utafiti na Machapisho kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Prof. Robinson Mdegela, ambaye alizungumza kwa niaba ya taasisi za utafiti zilizoshiriki, ameishukuru TFRA kwa kuwashirikisha katika kikao hicho.
Ameeleza kuwa Mamlaka ina jukumu kubwa la kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo zilizo hakikiwa ubora na zinazokidhi mahitaji ya udongo na mazao kwa wakulima.
Aidha, Prof. Mdegela amewapongeza wajumbe kwa uwazi wao katika mjadala na kuahidi kuwasilisha maazimio yaliyofikiwa kwa uongozi wake kwa ajili ya utekelezaji. Pia, ameahidi kuendelea kukusanya maoni kutoka kwa wahadhiri watafiti ili kuboresha zaidi ushirikiano kati ya TFRA na taasisi za utafiti.
Akizungumza kwa niaba ya TFRA, Afisa Udhibiti Ubora Mkuu na Kaimu Meneja wa usajili kutoka TFRA, Bw. Gerold Nganilevanu, amezishukuru taasisi shiriki kwa ushirikiano wao tangu mwanzo wa kikao hadi mwisho. Pia, ametoa rai ya kuendeleza ushirikiano huo katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku ya Mamlaka.
Taasisi za utafiti wa kilimo zilizoshiriki kikao hicho ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Utafiti wa Zao la Kahawa (TACRI), Taasisi ya Utafiti wa Zao la Tumbaku (TORITA), na Taasisi ya Utafiti wa Zao la Chai (TRIT).
Post Comment
No comments