SUZA, APRM TANZANIA KUSHIRIKIANA KUIMARISHA UTAWALA BORA
Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kimeeleza dhamira yake ya kushirikiana na Taasisi ya Mpango wa Hiari wa Kujitathmini katika Vigezo vya Utawala Bora Barani Afrika (APRM) Tanzania katika kufanya tathmini za utawala bora kwa maslahi ya taifa.
Makamu Mkuu wa SUZA, Prof. Moh’d Makame Haji, amesema kuwa taasisi hizo mbili ni nguzo muhimu kwa taifa katika kuhakikisha tathmini za utawala bora zinafanyika kwa ufanisi. Amesema tathmini hizo zitasaidia kuangazia maeneo ambayo serikali inafanya vizuri na kuyaendeleza, pamoja na kubaini changamoto zinazohitaji mikakati ya kuzitatua.
Akizungumza katika mkutano na ujumbe wa APRM Tanzania waliotembelea makao makuu ya chuo hicho Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, Prof. Makame amesema kuwa SUZA ina nafasi kubwa ya kushirikiana na APRM kutokana na kuwa na wataalamu wabobezi wa ngazi mbalimbali. Ameeleza kuwa chuo hicho kina mipango ya muda mfupi na mrefu ya kuhakikisha kuwa michango yao inazalisha mawazo chanya kwa maendeleo ya taifa.
Amebainisha kuwa SUZA imefungua milango yake kwa APRM ili kushirikiana katika maeneo mbalimbali kupitia mkataba wa mashirikiano unaotarajiwa kusainiwa karibuni, jambo litakalosaidia kuboresha mchakato wa tathmini za utawala bora kwa misingi ya kitaalamu na kwa maslahi ya wananchi.
Kwa upande wake, mjumbe wa Baraza la Usimamizi la Taifa la APRM Tanzania, Bw. Said Ali Muhammed, amesema kuwa waasisi wa Bara la Afrika walikuwa na maono makubwa ya kuhakikisha Afrika inaimarika katika masuala ya utawala bora kwa maendeleo endelevu. Ameeleza kuwa moja ya majukumu makuu ya APRM ni kufanya tathmini za hali ya utawala bora nchini, jambo linalohitaji ushirikiano wa karibu na taasisi za kitaaluma kama SUZA.
Amefafanua kuwa SUZA na APRM wamekuwa na uhusiano wa muda mrefu, ambapo chuo hicho kilishiriki kikamilifu katika tathmini ya kwanza ya utawala bora nchini Tanzania. Katika mchakato huo, SUZA ilitoa wataalamu waliotoa mchango mkubwa katika kuandaa ripoti ambayo ilitajwa kuwa mfano bora si tu barani Afrika, bali pia iliiwezesha Tanzania kujenga taswira chanya kimataifa.
Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Bw. Lamau Mpolo, amesema kuwa vipaumbele vya taasisi hiyo kwa sasa ni kufanya tathmini za Ndani za utawala bora, kuhamasisha jamii, kurejea muundo wa taasisi, na kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo vyuo vikuu nchini. Ameeleza kuwa tathmini hizo, zinazozingatia vigezo na miongozo ya kimataifa, zina umuhimu mkubwa kwani hutumika kama rejea muhimu katika masuala ya utawala bora.
Amesema kuwa mpango wa APRM unawagusa wananchi wengi kwa kuwawezesha kushiriki katika mchakato wa kutoa ushauri kwa serikali yao, kwa kuzingatia dhana ya utawala shirikishi inayoungwa mkono duniani kote.
Post Comment
No comments