CUF YALAANI KAULI YA CCM DHIDI YA CHADEMA, WATOA ANGALIZO
CUF- Chama Cha Wananchi kimepokea kwa mshangao na mshtuko mkubwa Kauli iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) juu ya mikakati haramu ya kutumia virusi vya Ebola na Mpox kuzuia Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Kauli hiyo ya kuhofisha iliyotolewa na Katibu wa Uenezi wa CCM ndugu Amos Makalla bila shaka ni Kauli ya Chama chake kwa kuzingatia wadhifa wake na kwa kuzingatia ukweli kwamba hakuna kiongozi yeyote wa juu zaidi wala chombo chochote ndani ya CCM kilichojitokeza kuikana kwamba si kauli ya chama chao. Hata Mwenyekiti wa CCM Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa kimya kuashiria kwamba ndugu Amos Makalla alikiwakilisha vyema chama chake.
Kauli hiyo kwa vyovyote vile, itakuwa na athari hasi kwenye Mchakato wa Uchaguzi Mkuu, hususan kwenye mikutano ya Kampeni na zoezi la Upigaji Kura kutokana na kujenga hofu na taharuki miongoni mwa wananchi.
Kwa kuwa kauli hiyo ya CCM ilitolewa kwenye mkutano wa hadhara, tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kumhoji ndugu Makalla ili kubaini endapo Kauli hiyo aliyoitoa kwa niaba ya chama chake ina ukweli wowote. Katika kushughulikia suala hili na kuondoa hali ya hofu na taharuki inayoenea kwa kasi kote nchini, pamoja na vyombo vingine, vyombo vifuatavyo vinabeba majukumu mahususi kama ifuatavyo:-
1. Jeshi la Polisi linapaswa kushughulikia Jinai ambayo haikwepeki kwenye suala hili. Endapo Kauli ya CCM ni ya kweli bila shaka CHADEMA watakuwa wahusika wa Jinai na endapo Kauli hiyo ni uzushi na kupakana matope, hakutakuwa na namna ya kumuepusha Makalla na chama kilichomtuma kutoa kauli hiyo na Jinai;
2. Ikibainika kufuatia (1) hapo juu kwamba Shutuma dhidi ya CHADEMA zina ukweli na Mahakama ikathibitisha hivyo, Msajili wa Vyama vya Siasa awajibike kwa Mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa;
3. Ikibainika kwamba kauli ya CCM ni uzushi, pamoja na jinai tuliyoitaja (1) hapo juu, Msajili wa Vyama awajibike dhidi ya Makalla na chama chake kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa; na
4. Pamoja na hatua za Kisheria zilizotajwa hapo juu, Chama kitakachokutwa na hatia ni lazima kijitokeze hadharani na kuwaomba radhi watanzania kwa lengo la kujaribu kuwarejeshea utulivu na kuzima hofu na taharuki, kama moja ya njia muhimu za kunusuru Uchaguzi Mkuu.
CUF- Chama Cha Wananchi kinatoa wito kwa vyombo vilivyotajwa hapo juu na vyombo vingine vinavyohusika moja kwa moja katika kulishughulikia jambo hili haraka sana bila ya kuruhusu kukomaa kwa hofu na taharuki na hatimaye kuathiri mwitikio wa wapiga kura kwenye mikusanyiko ya Uchaguzi Mkuu.
Post Comment
No comments