TAARIFA KUTOKA KIKAO CHA DHARURA CHA KAMATI YA UTENDAJI CUF TAIFA, AMBAYO IMEKUTANA LEO NA KUONGOZWA NA MAALIM SEIF MJINI ZANZIBAR.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati ya Utendaji ya Taifa ya
THE CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi) imekutana katika kikao cha
dharura cha siku moja leo hii katika Makao Makuu ya Chama, mjini Zanzibar chini
ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo, ambaye ni Katibu Mkuu wa Chama, Maalim Seif
Sharif Hamad.
Kikao hicho kilikuwa na ajenda
moja tu ambayo ni Maandalizi ya Uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi za Madiwani 22
kwa upande wa Tanzania Bara na nafasi ya Ubunge wa jimbo la Dimani kwa upande
wa Zanzibar.
Kamati ya Utendaji ya Taifa imepitisha
ratiba ya uchaguzi wa ndani ya Chama kwa ajili ya kuwapata wagombea wa CUF
katika nafasi hizo ambayo itasambazwa katika Wilaya na Kata husika kufuatia
kukamilika kwa kikao hiki.
Ikumbukwe kwamba CUF bado ni
sehemu ya UKAWA na suala hilo lilipitishwa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama
uliofanyika 23 – 27 Juni, 2014 ambacho ndicho chombo cha juu kabisa na chenye
maamuzi ya mwisho katika Chama. Kwa msingi huo, hakuna mtu yeyote mwenye uwezo
wa kutengua uamuzi huo isipokuwa Mkutano Mkuu wa Taifa wenyewe tu. Kwa sababu
hizo, CUF inaendelea na mazungumzo na vyama vyengine vinavyounda UKAWA kuona
namna bora ya kushiriki chaguzi hizi itakayohakikisha kuwa tunaibwaga CCM.
Katika hatua nyengine, Kamati
ya Utendaji ya Taifa imeshangazwa na kauli ya ajabu ya Mkurugenzi wa Uchaguzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu Ramadhani K. Kailima, kusema kwamba
wagombea wa CUF katika uchaguzi huo ni lazima fomu zao za uteuzi zithibitishwe
na kutiwa saini na Yule aliyemwita Mwenyekiti anayetambuliwa na Msajili wa
Vyama vya Siasa pamoja na Katibu Mkuu wa Chama, na kwamba kinyume na hivyo,
wagombea hao hawatotambuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Kauli hii ya Ndugu Kailima
inathibitisha kwa mara nyengine kwamba vyombo na taasisi za Dola vinatumika
kikamilifu kupandikiza na kuchochea ule unaoitwa mgogoro ndani ya CUF kwa lengo
la kukihujumu Chama chetu. Masuala ya uteuzi wa wagombea na fomu za uteuzi wa
wagombea yanaongozwa na Sheria ya Uchaguzi na Kanuni za Uchaguzi. Ndugu Kailima
amekitoa wapi kifungu cha Sheria au Kanuni alichokitumia kuweka sharti hilo la
ajabu tena kwa chama kimoja tu? Mojawapo ya misingi ya sheria ni kutokuwepo kwa
ubaguzi katika utungaji na utekelezaji wa sheria. Huwezi kuwa na sharti
linalokihusu chama kimoja tu katika kuthibitisha uteuzi wa wagombea .
Picha kwa hisani ya Maharagande Mbarala
|
Masuala ya jinsi ya kuwapata
wagombea wa Chama yanayongozwa na Katiba ya Chama ya 1992 (Toleo la 2014) na
Kanuni za Uchaguzi wa ndani ya Chama. Fomu za uteuzi wa wagombea kutoka Tume ya
Taifa ya Uchaguzi siku zote huthibitishwa na Katibu wa Chama wa ngazi inayohusika
na kwa Ubunge na Madiwani imekuwa ni Katibu wa Wilaya. Kitendo cha Ndugu
Kailima kuja na sharti lake kutoka mfukoni kuihusu CUF katika chaguzi hizi
ndogo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za uchaguzi na ni mwendelezo wa
hujuma za Dola na taasisi zake dhidi ya CUF kwa kumtumia mtu anayeitwa Ibrahim
Lipumba. CUF haitozikubali hujuma hizi na itazilinda na kuzitetea haki zake za
kikatiba na kisheria kikamilifu.
Mwisho kabisa, Kamati ya
Utendaji ya Taifa inawapongeza wanachama wa CUF kwa ujasiri wao wa kukilinda
Chama chao kwa mapenzi na nguvu zao zote dhidi ya njama za wanasiasa muflisi
ambao wamekubali kujiuza kwa bei rahisi kutumikia watawala wakidhani wanaweza
kukivuruga Chama hiki. Kamati ya Utendaji ya Taifa inawahakikishia wanachama wote
wa CUF kwamba iko imara na itaendelea kufanya kazi ya kukilinda na kukitumikia
Chama na wajue kwamba tutashinda MAPAMBANO HAYA.
HAKI
SAWA KWA WOTE
Kamati
ya Utendaji ya Taifa
THE
CIVIC UNITED FRONT (CUF – Chama Cha Wananchi)
13
Desemba, 2016
No comments