Breaking News

WABUNGE WAIPONGEZA SERIKALI KWA KUTOA BILIONI 10.4 KUJENGA MAKAO MAKUU MAPYA YA MAMLAKA YA HIFADHI YA NGORONGORO

Na Mwandishi wetu - Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wameipongeza na kuishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga jumla ya shilingi 10,474,526,694.25 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro pamoja na nyumba tatu za kuishi viongozi wa mamlaka hiyo.

Wakizungumza mara baada ya kutembelea ujenzi wa makao makuu mapya ya mamlaka hiyo unaoendelea katika mji wa Karatu Mkoani Arusha baadhi ya wabunge hao wamesema uamuzi wa serikali ya awamu ya sita ya kuendelea kutoa fedha na kujenga ofisi hizo utasaidia watumishi wa mamlaka hiyo kufanya kazi katika mazingira mazuri.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Timotheo Mnzava amesema kinachotakiwa kwa sasa ni wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha kuwa miundombinu hiyo pamoja na mingine inayosimamiwa na wizara hiyo inamalizika kwa wakati na kuanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mnzava amesema kamati inataka kuona ujenzi wa miundombinu hiyo unakamilika kwa wakati huku akisisitiza thamani ya fedha katika utekelezaji wa mradi huo na ubora wa majengo yanayojengwa ili yakidhi mahitaji yaliyotarajiwa.

Wabunge mbalimbali wa kamati hiyo waliochangia kuhusu mradi huo katika kikao cha majumuisho mara baada ya ziara hiyo wamesema ni matarajio yao kuona kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati ili uanze kutumika
Waziri wa Malisili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi H. Chana ametoa shukrani kwa wabunge hao kutokana na kuisimamia na kuishauri wizara, na kusema kuwa maelekezo yote ya kamati hiyo yatafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuisimamia menejimenti ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika ujenzi wa mradi huo hatua kwa hatua.

Mradi wa ujenzi wa jengo la utawala la mamlaka hiyo, nyumba ya Kamishna wa Uhifadhi na nyumba za manaibu Kamishna umefikia asilimia 85 ya ujenzi na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu.







No comments