HAKUNA MRADI WA MAJI AMBAO UMESIMAMA: MSIGWA

Pwani - Imeelezwa kuwa hadi sasa hakuna mradi wowote wa maji ambao umesimama na lengo lake ni kuhakikisha maisha ya Watanzania yanakuwa mazuri na kasi kubwa inaendelea kuhakikisha huduma hiyo inamfikia kila mwananchi.

Greyson Msigwa ambaye ni Msemaji wa Serikali amebainisha hayo leo mkoani Pwani, mbele ya waandishi wa habari na kusisitiza kwamba utekelezaji huo unafanyika ili kuboresha maisha ya Mtanzania kwa kuhakikisha anapata maji safi na kuimarisha sekta ya nishati kwa maendeleo endelevu.

Pia amekumbusha kwamba Machi 9, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua mradi mkubwa wa maji katika Wilaya ya Same, ambapo Shilingi bilioni 406 zimewekezwa. Mradi huo, ambao umekamilika kwa asilimia kubwa, utawanufaisha wakazi wa Same, Mwanga na Korogwe kwa kuboresha upatikanaji wa maji safi katika maeneo hayo.
Mbali na mradi huo, serikali pia inatekeleza mradi wa Bwawa la Kidunda kwa gharama ya Shilingi bilioni 335.9. Bwawa hili litasaidia kuboresha upatikanaji wa maji kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, huku likitarajiwa pia kuzalisha megawati 20 za umeme ambazo zitaunganishwa kwenye gridi ya taifa. Mradi huu umezingatia usalama wa wananchi wanaozunguka bwawa hilo, huku zaidi ya wakazi 7,000 wa vijiji vya Kidunda na Mkulazi wakitarajiwa kunufaika moja kwa moja na maji yatakayopatikana. Kwa sasa, serikali inaendelea kusanifu njia bora za kusambaza maji kwa wananchi wa maeneo hayo.

Katika juhudi za kuhakikisha maji yanapatikana kote nchini, serikali inaendelea na mradi mkubwa wa kusambaza maji kutoka Ziwa Victoria hadi mkoa wa Dodoma, hatua itakayoboresha upatikanaji wa maji safi katika mji mkuu na maeneo jirani.

Aidha, serikali inatekeleza mpango kabambe wa miradi ya maji katika miji 28, ambapo zaidi ya Watanzania laki sita watanufaika. Kati ya miradi hiyo, maendeleo ya utekelezaji ni kama ifuatavyo:
Pangani - Muheza (63%)
Kilwa Masoko - Nanyumbu (70%)
Ifakara - Njombe - Chunya (28%)
Singida - Manyoni - Chemba (14%)
Rambo - Kaliua - Sikonge - Songwe (50.5%)
Geita - Chato (50.5%)
Mafinga (16%)
Rorya - Tarime (12%)
Songea (5%)

No comments