TEMEKE YAPANDA MITI 482 KUADHIMISHA SIKU YA UPANDAJI MITI

Dar es Salaam – Katika kuadhimisha Siku ya Upandaji Miti, Ofisi ya Mhifadhi Wilaya ya Temeke kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, wananchi na wanafunzi, wamefanya zoezi kubwa la upandaji miti katika Shule ya Msingi Ushirika, Kata ya Yombo Vituka.

Zoezi hilo lililojaa hamasa liliendeshwa leo, likihudhuriwa na wadau mbalimbali wa mazingira na kuongozwa na Mgeni Rasmi, Diwani wa Kata ya Yombo Vituka, Mheshimiwa Fulugence Lwiza. Akihutubia hadhira, Diwani Lwiza alisisitiza wajibu wa kila mwananchi katika kuhifadhi mazingira kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kwa mujibu wa taarifa za waandaaji, jumla ya miti 482 ya kivuli ilipandwa katika eneo hilo kama sehemu ya jitihada za wilaya hiyo kuhakikisha kunakuwepo na uoto wa kutosha unaosaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Kaimu Mhifadhi Wilaya ya Temeke, CO Sunday Nachuli, aliwahimiza wananchi kufika katika bustani ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuchukua miche ya miti bure, hasa katika msimu huu wa mvua.
“Tunazo miche ya kutosha na tunaitoa bure kwa wananchi wote. Ni jukumu letu sote kuhakikisha miti hii inatunzwa na kuangaliwa mara kwa mara,” alisema Nachuli, akiongeza kuwa kutakuwa na ukaguzi wa mara kwa mara kufuatilia maendeleo ya miti iliyopandwa.

Maadhimisho haya yaliyopewa kauli mbiu “Tumerithishwa, Tuwarithishe”, yamepokelewa kwa hamasa kubwa na yameacha alama muhimu katika jitihada za Manispaa ya Temeke kuendeleza mazingira bora na endelevu kwa jamii yote.

No comments