KAFULILA AANISHA DAWA YA DENI LA TAIFA

Na Mwandishi Wetu - Mfumo wa utekelezaji miradi ya maendeleo kwa njia ya ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi utawezesha kasi ya ongezeko la deni la taifa kupungua.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo imeonesha deni la taifa limeongezeka hadi kufikia shilingi trilioni 97.35 kwa mwaka wa fedha 2023/24 kutoka shilingi trilioni 82.25 mwaka 2022/23.

Kwa mujibu wa CAG, Charles Kichere alisema ongezeko la deni hilo ni sawa na asilimia 18.36, ambapo deni la nje shilingi trilioni 65.40, huku deni la ndani likifikia shilingi trilioni 31.95.

Katika ripoti alizowasilisha kwa Rais Samia Alhamisi iliyopita, CAG Kichere alibaini kuwa ukaguzi uliofanywa katika mashirika 12 kati ya 217 uligundua matumizi mabaya ya shilingi bilioni 371.42 . 

Alisema fedha hizo zilitumika katika shughuli ambazo hazikutoa thamani yoyote kwa taasisi husika za umma, na akaitaka serikali kushughulikia kasoro hizo.

Akifafanua kuhusu deni hilo, Kafulila alisema kwa hali ilivyo kwa sasa ni muhimu serikali kuweka nguvu kwenye miradi ya ubia ambayo itahusisha sekta ya umma na binafsi, kwa kuwa serikali itaweza kupunguza mzigo wa kutekeleza miradi mbalimbali kwa fedha za kukopa.

Kafulila amesema ubia kati ya sekta ya umma na binafsi unaweza kusaidia nchi kufadhili mipango yake ya maendeleo huku ikipunguza utegemezi wa mikopo ya kimataifa.

"Mimi naamini tukitumia mifumo ya PPP nchi inaweza kupunguza utegemezi na hizi taarifa za deni la taifa kuongezeka zitapungua kama sio kuisha kabisa. Duniani kwa sasa miradi mikubwa inatekelezwa njia ya ubia na ufanisi ni mkubwa," alisema.

Alisema kuwa ingawa deni la Tanzania bado linadhibitika ikilinganishwa na mataifa jirani ya Afrika Mashariki, PPPs zinatoa njia mbadala endelevu kwa ufadhili wa miradi mikubwa ya maendeleo badala ya kutegemea mikopo mizito.

"Kuongeza mtaji kupitia ubia wa sekta ya umma na binafsi huongeza mapato ya kodi kwa kuwa miradi hii inaleta mapato.

Pia hupunguza gharama ambazo zingebebwa kikamilifu na serikali. Kwa kutumia rasilimali, ufanisi, na teknolojia ya sekta binafsi, Tanzania inaweza kufanikisha ukuaji endelevu hali ambayo mataifa mengi sasa yanaitambua," alisema.

Kafulila alielezea lengo la Tanzania kukuza uchumi wake kutoka Dola za Marekani bilioni 85 hadi Dola bilioni 700 litafanikiwa.

Mkurugenzi huyo alisema lengo la uchumi wa Dola bilioni 700, Tanzania itazidi Pato la Taifa la Afrika Kusini, ambalo kwa sasa ni Dola bilioni 405 na kwamba hilo haliwezi kufanikishwa kwa kutegemea mikopo na kodi pekee na ubia wa kimkakati ni muhimu.

Kafulila alisema kwa sasa, PPPC inasimamia zaidi ya miradi 84 ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, ikiwa ni pamoja na mradi wa barabara ya Kibaha-Chalinze wenye thamani ya Dola milioni 340 na ujenzi wa barabara ya mzunguko yenye thamani ya Dola bilioni 1. 

Kafulila alisema anaamini hatua dhidi ya ufisadi zitaiwezesha nchi kuokoa fedha nyingi na hivyo kujiweka katika nafasi bora ya kufanikisha malengo yake bila kutegemea mikopo ya kimataifa kwa kiasi kikubwa.

"Nakubaliana kuwa vita dhidi ya ufisadi huongeza ufanisi na uwajibikaji. Unapoboreshwa ufanisi na uwajibikaji, unaokoa hasara ambazo zingesababishwa na kasoro hizo. Hili ni jambo halisi."

Kafulila pia alitumia fursa hiyo kueleza umuhimu wa kampuni za ndani kushiriki katika miradi ya PPP ambayo serikali inapanga kutekeleza, akieleza kuwa mamlaka zinapaswa kutilia mkazo jambo hili si kwa sababu za kisiasa pekee, bali pia kwa sababu za kiuchumi.

"Unapojenga uchumi kwa kutumia ubia wa ndani, kwanza, unaingiza mtaji ndani ya nchi kwa sababu washirika hawa ni wa ndani. Kile wanachopata, wanakizalisha upya hapa, tofauti na wawekezaji wa kigeni, ambao wangerejesha sehemu kubwa ya mapato yao nje ya nchi," alisema Kafulila.

"Sasa, katika tathmini, kwa mujibu wa sheria, wakati wa kuchunguza kampuni kwa ajili ya mradi, ikiwa kampuni ya kigeni inashindana na kampuni ya ndani, kampuni ya ndani inapewa kipaumbele—si kwa sababu za kisiasa pekee, bali pia kwa sababu za kiuchumi, kwani fedha zitazunguka ndani ya nchi," aliongeza.

No comments