TFRA, NLUPC WATEKELEZA ZOEZI LA URASIMISHAJI WA MASHAMBA SONGWE
Wakulima wa kijiji cha Kanga wakiendelea kuweka saini kwenye hati zao ikiwa ni hatua ya sita ya zoezi la kumilikishwa ardhi kisheria baada ya kuhakiki taarifa zao kabla ya kuzichukua rasmi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, akizungumza na wakulima wa kijiji cha Kanga kilichopo katika Wilaya ya Songwe mkoani Songwe wakati wa zoezi la uhakiki wa hati miliki za kimila za mashamba ya wakulima wa Kijiji hicho leo tarehe Mosi Aprili, 2025.
Afisa tarafa wa Tarafa ya Songwe, Godwin Kaunda, akizungumza na wakulima wa kijiji cha Kanga kilichopo Wilaya ya Songwe mkoani Songwe waliofika kwa ajili ya kuhakiki taarifa za hati miliki za mashamba tukio lilifanyika kwenye ofisi za kijiji tarehe 1 Aprili, 2025
Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiaji wa Matumizi ya Ardhi kutoka NLUPC Rehema Kishoa,(aliyesimama meza kuu) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kanga wakati wa zoezi la uhakiki wa Hati za mashamba unaofanyika kijijini hapo kuanzia tarehe Mosi Aprili, 2025 mpaka pale litakapokamilika kwa wakulima kupewa hati zao
Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Bw. Joel Laurent (kulia) akiita majina ya wanakijiji kwa ajili ya kusogea mezani ili kuhakiki taarifa zao kwenye hati miliki za kimila za mashamba wanayomiliki katika kijiji cha Kanga, Halmashauri ya Wilaya ya Songwe mkoani Songwe tarehe Mosi Aprili, 2025
Wakulima wa kijiji cha Kanga wakiendelea kuweka saini kwenye hati zao ikiwa ni hatua ya sita ya zoezi la kumilikishwa ardhi kisheria baada ya kuhakiki taarifa zao kabla ya kuzichukua rasmi.
Wakulima wakisikiliza maelekezo ya serikali kabda ya kuanza rasmi kwa zoezi la kuhakiki taarifa zao kabla ya kumilikishwa hati miliki za kimila za mashamba wanayoyamiliki katika kijiji cha Kanga Wilayani Songwe mkoani Songwe.
Songwe - Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent, ameridhishwa na hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa zoezi la urasimishaji wa mashamba kwa wakulima waliosajiliwa mkoani Songwe aliposhiriki kwenye zoezi la uhakiki wa hati miliki za kimila za mashamba ya wakulima wa Kijiji cha Kanga kilichopo katika Wilaya ya Songwe mkoani Songwe.
Laurent ameonesha kuridhishwa na zoezi hilo leo tarehe Mosi Aprili, 2025 alipotembelea kijiji hicho kujionea utekelezaji wa zoezi la uhakiki wa hati miliki za kimila za mashamba ya wakulima 3,098 wa vijiji vya Gua, Kapalala, Kanga na Galula linalotekelezwa kwa awamu ya kwanza katika wilaya ya Songwe kwa ushirikiano baina ya TFRA, NLUPC na Halmashauri ya Wilaya ya Songwe.
Zoezi hilo linaenda sambamba na uhuishaji na usajili wa wakulima, uchukuaji wa taarifa kwa ajili ya upatikanaji wa kadi janja na uandikishaji wa wakulima kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vya taifa (NIDA)
Mkurugenzi Mtendaji huyo ametoa rai kwa wakulima wote waliosajiliwa kujihusisha na kilimo chenye tija kwa kufuata kanuni bora za kilimo na kutumia pembejeo ili kuongeza tija ya uzalishaji.
Aidha Bw. Laurent amewahakikishia wakulima kuwa ni nia ya serikali kuhakikisha wakulima waliosajiliwa na kukidhi vigezo wanapatiwa hati miliki na kadi janja za utambulisho wa mkulima.
Hatua ambayo itamsaidia mkulima kunufaika na umiliki wa ardhi na fursa mbalimbali zikiwemo za kifedha na mikopo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NLUPC , Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiaji wa Matumizi ya Ardhi, Rehema Kishoa, amesema ukamilishaji wa hatua hii utawezesha wakulima kukabidhiwa hati miliki za kimila zitakazowawezesha kuongeza usalama wa ardhi na kuiwezesha TFRA
kupata taarifa sahihi za mashamba ya wakulima ili kuboresha utoaji wa huduma za pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea na mbegu kwa bei ya ruzuku .
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kanga, Mhe. Erick Kihinda, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwapa kipaumbele wakulima wa Mkoa wa Songwe kupimiwa mashamba yao na kupewa hati miliki zitakazowafaa katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususan katika kuendeleza kilimo cha mazao mbalimbali yakiwemo alizeti, mahindi na ufuta.
Aidha Kihinda amempongeza Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe kwa usimamizi thabiti wa sekta ya kilimo ambapo wakulima wanashuhudia mabadiliko makubwa yanayofanyika kwa lengo la kuinua uchumi wa taifa na mwananchi mmoja mmoja.
Naye, Afisa Tarafa wa Tarafa ya Songwe, Godwin Kaunda, amesema serikali inatekeleza majukumu yake kwa wakati kama inavyoahidi.
“Ni mwaka jana tu tulianza zoezi la upimaji wa mashamba lakini leo tunakwenda kuhakiki hati zetu. Urasimishaji wa ardhi unaleta usalama kwa wakulima na kusaidia kuondoa migogoro ya mipaka iliyokuwepo hapo awali’’. amemaliza kusema Kaunda.
Post Comment
No comments