DKT. MPANGO MGENI RASMI TUZO YA TAIFA MWALIMU NYERERE UANDISHI BUNIFU 2025.
Waziri wa elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa. Adolf Mkenda akifafanua jambo juu ya maandalizi ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu zitakofanyika Aprili 13, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
Dar es salaam - Makamu wa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania dokta Isdor Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu zitakofanyika Aprili 13, 2025 katika ukumbi wa Mikutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC) jijini Dar es salaam.
Akizungumza mapema leo, Aprili 7, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu na Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia kubwa na ukizingatia siku hiyo Aprili 13 ni siku ya kumbukizi ya kuzaliwa, Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere.
"Kwa kutambua uzito wa tuzo hiyo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni makamu wa Rais inadhihirisha namna Serikali inavyotambua na kuweka uzito katika tuzo hiyo ya Uandishi Bunifu ambayo kwa njia moja ama nyingine inasaidia kukuza lugha ya Kiswahili kutokana na Waandishi shindani kutumia lugha hiyo katika kazi zao". Alisema Prof. Mkenda.
Alisema Tuzo ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ni miongoni mwa njia bora za kuenzi fikra, falsafa na maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye aliweka msingi wa matumizi na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili kama nyenzo ya elimu, umoja na maendeleo ya jamii ya Watanzania.
“Tuzo hii ni heshima kwa Mwalimu Nyerere lakini pia ni jukwaa mahsusi kwa waandishi chipukizi na wakongwe kuonesha umahiri wao katika nyanja mbalimbali za uandishi kama vile riwaya, ushairi, hadithi za watoto na tamthiliya,”. Alisema Prof. Mkenda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya uratibu wa Tuzo, Profesa Penina Mlama amesema majaji tayali wamekamilisha kazi ya kusoma na kupitia miswada yote iliyowasilishwa na kupata orodha ya wateule waliopendekezwa kuwania tuzo hiyo.
Alisema tayari kazi mbili za washindi zimechapishwa na kazi ya tatu zipo katika hatua za mwisho kukamilika ambapo Mshindi wa kwanza Tuzo za Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu kwa mwaka 2025 atazawadiwa milioni 10 pamoja na cheti. mshindi wa pili milioni 7, mshindi wa tatu milioni 5, na mshindi wanne hadi wa 10 watapatiwa Vyeti kutambua ushiriki wao.
Post Comment