MWENYEKITI WA NLD AHITIMISHA ZIARA YA UJENZI WA CHAMA ZANZIBAR
Chaani Zanzibari
Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha NLD, Mhe. Mfaume Khamis Hassan, akiwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Mhe. Doyo Hassan Doyo, wamemalizia ziara yao ya ujenzi wa chama unguja Zanzibari kwa kutembelea ujenzi wa Msikiti wa Chaani Ugomani, Shehiya ya Masingini. Katika ziara hiyo, Mhe. Mfaume, ambaye pia ni mkazi wa Chaani, alimueleza Mhe. Doyo kuhusu jinsi chama cha NLD kilivyochangia na kujitolea katika ujenzi wa msikiti huo.
Mhe. Mfaume alisisitiza kuwa chama cha NLD kitaendelea kuchangia huduma mbalimbali za kijamii kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali za kuwaletea wananchi maendeleo. Alisema, "Chama cha NLD hatutoishia kuchangia msikiti tu, hata tukialikwa kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa, tutafanya hivyo na kutoa kile tutakachojaliwa. Lengo letu ni kuwa na jamii ya Watanzania yenye maadili na hofu ya Mungu."
Wananchi wa Chaani wameshukuru mwenyekiti na chama chake cha NLD kwa mchango wao wa hiari na kuomba viongozi hao waendelee kuwa na moyo huo wa kujitolea katika shughuli za kijamii.
Pia Mhe. Doyo, kwa upande wake, alitoa mwito kwa viongozi wa vyama vya siasa kujitolea katika shughuli za ibada, akieleza kuwa dini ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya nchi, " kupitia nyumba za ibada, tumepata viongozi mbalimbali waadilifu.
Pia amewapongeza wananchi wa Chaani kwa ujasiri wao wa kuwafata na kuwahusisha viongozi wa NLD katika shughuli za kijamii kama ujenzi wa nyumba ya ibada, huku akizisihi taasisi nyingi zaidi kushiriki katika kuchangia maendeleo ya jamii. Chama cha NLD kimemaliza ziara ya siku nne unguja kabla ya kuelekea Tanga na Pemba.
No comments