Breaking News

VIONGOZI WA CHAMA CHA NLD WATEMBELEA MIRADI ZANZIBAR

Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Mfaume Khamis Hassan, akiambatana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Mhe. Doyo Hassan Doyo, leo tarehe 13-09-2024 walitembelea mradi wa umwagiliaji maji katika Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Mhe. Mfaume amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussen Ally Mwinyi, kwa jitihada zake za kuendeleza miradi ya maendeleo. Ameipongeza serikali kwa kufanikisha mradi wa bwawa la kuhifadhi maji, unaowanufaisha wananchi hususan wananchi wanaolima kwenye bonde Chaani Ketwa kwa kuwezesha kilimo cha umwagiliaji.

"Naipongeza serikali kwa kutoa eneo hili bure ili wananchi wa Kaskazini waweze kufanya kilimo cha kisasa na chenye tija. Hii ni hatua kubwa kwa maendeleo ya wananchi," alisema Mhe. Mfaume Mwenyekiti wa NLD Taifa.

Pia Katibu mkuu wa National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo alimpongeza Rais Hussen Ally Mwinyi kwa jitihada zake, huku akihimiza serikali kuongeza miradi mingine ili kupunguza tatizo la ajira visiwani Zanzibar. Ziara ya NLD inatarajiwa kuhitimishwa kesho, kabla ya kuelekea Tanga na Pemba.

No comments