WATAHINIWA 557,731 KUFANYA MTIHANI WA KUHITIMU KIDATO CHA NNE KESHO NOVEMBA 11, 2024
Jumla ya watahiniwa 557,731 wanatarajiwa kuanza kufanya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne kuanzia kesho Jumatatu Novemba 11 hadi Novemba 15, 2024 kati yao 529,321 ni wa shule na watahiniwa wa kujitegemea ni 28,410.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dkt. Said Mohamed amesema hayo leo Novemba 10, jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mtihani huo.
Dkt Mohamed amesema katika watahaniwa wa shule 557,731 waliosajiliwa kufanya mtihani huo wavulana ni 250,562 sawa na asilimia 47.34 na wasichana ni 278,759 sawa na asilimia 52.66 na
Mtihani huo utafanyika katika shule za sekondari 5585 na vituo vya watahiniwa wa kujitegemea ni 961 .
“Watainiwa wa shule wenye mahitaji maalum 1,088 waliosajiliwa kati yao 601 ni wenye uoni hafifu, 56 ni wasioona, 209 wenye ulemavu wa kusikia, 39 ni wenye ulemavu wa akili na 183 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwili,”. Alisema Dkt. Mohamed
Alisema Watahiniwa wa kujitegemea 28,410 wamesajiliwa kati yao wavulana ni 11,167 sawa na asilimia 39.31 na wasichana 17,243 sawa na asilimia 60.69 huku kwa wenye mahitaji maalum wakiwa 18 kati yao mwenye uoni hafifu ni mmoja, wasioona 16 na mwenye ulemavu wa viungo mmoja.
Dkt. Mohamed alibainisha kuwa maandalizi yote kwa ajili ya mtihani yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa mtihani ,vijitabu vya kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mitihani husika katika mikoa yote Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha Dkt. Mohamed ametoa wito kwa kamati za mitihani za mikoa na Halmashauri kuhakikisha usalama wa vituo vya mitihani unaimarishwa na vinatumika kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Baraza.
“Kwa upande wa wasimamizi walioteuliwa kusimamia mtihani wahakikishe wanafanya kazi yao ya usimamizi kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. ”Alisema Dkt. Mohamed na kuongeza kuwa
"Kwa upande wa watahiniwa, Baraza hilo limewataka kufanya mitihani kwa kuzingatia kanuni za mitihani na kueleza kuwa halitarajii kuona mtahiniwa yoyote kujihusisha na vitendo vya udanganyifu".
Pia dkt.Mohamed aliongeza kuwa mtahiniwa yoyote atakayebainika kufanya udanganyifu, matokeo yake yatafutwa kwa mujibu wa kanuni za mtihani na Kwa upande wa wamiliki wa shule na wakuu wa shule, wanapaswa kutambua kuwa shule zao ni vituo maalumu vya mitihani hivyo kwa namna yoyote hawatakiwi kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mtihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mtihani huo.
Alisema baraza halitosita kukifuta kituo chochote cha mtihani endapo litajiridhisha pasipo shaka kuwepo wa matukio au vitendo vinavyohatarisha ukiukwaji wa usalama wa mtihani.
“Natoa wito kwa akuu wa shule wote kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao ya usimamizi kwa kuzingatia miongozo ya usimamizi iliotolewa na Baraza ikiwa ni pamoja na kuepeuka kuingilia usimamizi wa watahiniwa ndani ya vyumba vya mitihanii." Alisema Dkt. Mohamed
Alisema baraza pia linatoa wito kwa jamii, wazazi ma walezi kutoa ushirikiano kuhakikisha mtihani wa kidato cha nne na maarifa 2024 unafanyika kwa amani na utulivu.
“Wito kwa wananchi, wazazi pamoja na walezi kuhakkikisha kuwa hakuna mtu yoyote asiyehusika na mtihani anaingia kwenye maeneo ya shule katika kipindi chote cha mtihani kwani kwa kufanya hivyo tuatawezesha wanafunzi kufanya mtihanni kwa amani na utulivu". Alisema Dkt. Mohamed
No comments