TUKIFANYA KAZI KWA PAMOJA TUTAPATA WATALII WA KUTOSHA UKANDA WA KARIBE NA MAENEO JIRANI - BALOZI POLEPOLE
Na Hamis Dambaya,Havana
Balozi wa Tanzania nchini Cuba mheshimiwa Humphrey Polepole amesema kuwa amedhamiria kushirikiana na sekta zinazohusika katika masuala ya utalii nchini ili kuweza kutangaza utalii katika ukanda wa Karibe na maeneo ya nchi jirani ili kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuifungua nchi.
Mheshimiwa Polepole ametoa kauli hiyo alipokutana na ujumbe kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ambao walishiriki maadhimisho ya tamasha la Kiswahili la kimataifa lililomalizika jumamosi iliyopita jijini Havana nchini Cuba.
Mheshimiwa Polepole amesema kuwa tamasha la kimataifa la Kiswahili limekuwa na tija kubwa kwani amekutana na wadau wa sekta mbalimbali kutoka Tanzania ikiwemo wadau wa utalii ambapo kwa sasa yupo katika hatua za mwisho za kuhakikisha kuwa suala la utalii katika ukanda huo linakuwa ni moja ya ajenda zake ili kuongeza idadi ya watalii nchini.
“Kikubwa ninachokihitaji kutoka kwenu ni ushirikiano wa pamoja kuhakikisha kuwa mambo tunayoyapanga yanafanikiwa kwani eneo la Karibe na nchi jirani kutoka hapa ikiwemo Bahamas na maeneo mengine ni mahususi kwa kutembelewa na watalii wa kutosha hivyo mwaka ujao tutafanya jambo kubwa la kutangaza utalii,”alisema mheshimiwa Polepole.
Balozi huyo amepongeza uamuzi wa NCAA na TANAPA kwenda nchini Cuba kushiriki Tamasha hilo kwani kwa kufanya hivyo ni kupanua wigo wa shughuli za utalii na amezitaka taasisi hizo kuendelea kuwa wabunifu na kujaribu kuangalia nchi nyingine zinafanya nini ili kuongeza idadi ya watalii.
Kwa upande wake Kaimu naibu Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayeshughulikia uhifadhi,utalii na maendeleo ya jamii bi Victoria Shayo alimhakikishia balozi huyo kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii itafanyia kazi mapendekezo yatakayotolewa na ubalozi kupitia wizara ya mambo ya nje ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuongeza idadi ya watalii kama inavyoelekezwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Naye Afisa Utalii kutoka TANAPA Haika Bayona alimshukuru Balozi Polepole kwa kujitoa kuutangaza utalii wa Tanzania katika ukanda wa Karibe na maeneo jirani na kusema kuwa ushauri wake kuhusiana na masuala mbalimbali utasaidia kuboresha huduma za utalii katika maeneo ya hifadhi nchini.
Tamasha la kimataifa la Kiswahili nchini Cuba liliwakutanisha wadau kutoka nchi mbalimbali duniani ambapo taasisi zinazohusika na masuala ya utalii zilipata fursa ya kuzungumza na wadau hao ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vilivyopo nchini Tanzania.
No comments