Breaking News

WAZIRI UMMY: MGONJWA WA MARBURG ALIYEPONA ARUHUSIWA

Dar es salaam:
Mgonjwa  mmoja wa Marburg mwenye umri wa miaka (26) ameruhusiwa  akiwa na afya njema na jamii imetakiwa kumpokea vyema na kushirikiana nae katika shughuli zake. 

Hayo yameelezwa leo  jijini Dar es salaam na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akiongea na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa ugonjwa  wa Marburg ulioripotiwa Wilaya ya Bukoba vijijini mkoani kagera.

“Ninayo furaha  kubwa kuwajulisha kuwa  leo  tumemruhusu mgonjwa mmoja  mwanaume  mwenye umri  wa miaka (26) akiwa na afya njema, ni matumaini yangu jamii itampokea  vyema  na kushirikiana nae kama kawaida,  ni jambo la kumshukuru Mungu  kuwa hatujapata wagonjwa wapya wala vifo”.

Aidha, tangu kuripotiwa ugonjwa huu Machi 21, 2023 kufikia Aprili 4, 2023 jumla ya visa ni 8 na vifo 5.Waziri Ummy ameongeza kuwa wagonjwa wawili waliolazwa  wanaendelea vizuri na matibabu katika vituo maalumu vilivyoandaliwa.

Hata hivyo Waziri amesema kuwa jumla ya watu 212 waliotengamana na wagonjwa wamebainishwa na kati ya hao watu 35 wamemaliza siku 21 za uangalizi bila kuonesha dalili  zozote za ugonjwa .

“Hii ni ishara  nzuri sana kwetu, Wizara ya afya , serikali na taifa kwa ujumla kwa kuwa maambukizi ya Virus vya Marburg nchini yamedhibitiwa kwa wakati.Serikali bado inahimiza wananchi wote na hasa wa Mkoa wa kagera kuendelea kuchukua tahadhari, kudhibiti na kuzuia maamb ukizi mapya katika jamii”.

Vilevile Waziri Ummy amewahakikishia  watanzania na jamii ya Kimataifa kuwa Tanzania  ni salama hivyo wananchi waendelee  na shughuli na safari  bila hofu  yeyote na kwamba serikali bado inahimiza wananchi wote hasa wa mkoa wa Kagera kuendelea kuchukua tahadhari  kudhibiti ugonjwa na kuzuia maambukizi mapya katika jamii.

No comments