AREJESHEWA TABASAMU BAADA YA KUFANYIWA UPASUAJI REKEBISHI NA KUONDOLEWA UVIMBE KILO TANO ULIOMSUMBUA MIAKA 25
Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, mara baada ya kumpokea Bw. Kalume Agosti mwaka huu ambapo leo Septemba 20, 2024 akiruhusiwa kutoka hospital
Mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Dar es slaam (DCPC), bi Caren Mgoja akifafanua jambo juu ya mchamkato mzima na hatua zilizopitiwa tangu awali na chama hicho kuratibu matibabu ya kalume
Dar es Salaam
Mkazi wa Lindi, Bw. Kalume Kalume (41) aliyesumbuliwa na uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake kwa zaidi ya miaka 25, leo ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kufanikiwa kufanyiwa upasuaji rekebishi na watalaam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuondolewa uvimbe wenye uzito wa kilo tano.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Rekebishi na Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji Rekebishi Dkt. Laurean Rwanyuma aliyeongoza jopo la watalaam wenzake kumfanyia upasuaji uliodumu kwa saa nne, amesema baada ya uchunguzi wa kina kukamilika, iligundulika kuwa Bw. Kalume ana uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake hasa shingoni, begani na kifuani na ugonjwa huo unaitwa Plexiform Neurofibromatosis ambao matibabu yake ni kuondolewa kwa njia ya upasuaji ambapo Agosti 30 mwaka huu alifanyiwa upasuaji.
Dkt. Rwanyuma amesema, ugonjwa aliopata Bw. Karume siyo wa kuambukiza bali ni ugonjwa wa kuzaliwa nao ambao ameurithi kutoka kwa ama mmoja wa wazazi wake au wazazi wake wawili wenye ugonjwa huo ambao hushambulia mishipa ya fahamu na kujitokeza kwa njia mbalimbali.
Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji, Dkt. Rachel Mhaville akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, amesema mara baada ya kumpokea Bw. Karume Agosti mwaka huu, hospitali ilifanya jitihada za dhati kuhakikisha Bw. Kalume anaonwa na madaktari bingwa na kumfanyia vipimo mbalimbali ili kubaini mwenendo wa matibabu yake na kuwapongeza waandishi wa habari kumuibua mgonjwa huyo na kumleta hospitalini hapo kwani ndipo penye madaktari bingwa bobezi wa upasuaji rekebishi walioweza kumpa huduma stahiki na kumrejeshea mwonekano unaompa faraja na tabasamu.
Dkt. Mhaville amewaomba wasamaria wema kuendelea kujitokeza kuchangia huduma kwa watu wasiokuwa na uwezo akiwemo Bw. Karume ili kukamilisha malipo ya huduma alizopata kupitia namba ya malipo 994501766575 yenye jina Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Mapema mwakilishi wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Dar es slaam (DCPC), bi Caren Mgoja akizungumzia mchamkato mzima na hatua zilizopitiwa tangu awali amesema mara baada ya kupata taarifa za ugonjwa wa Kalume kutoka kwa mwandishi kalunde Mihambo chama kiliteua baadhi ya wajumbe na kuanza kufatilia kufatilia jambo hilo.
"Mara baada ya kupata taarifa kutoka kwa mwandishi mwenzetu juu ya uwepo mgonjwa DCPC tuliamua kuanza kufatilia kwa kufika alikokuwa anaishi na kuongea nae kisha kuanza utaratibu za matibabu ikiwa ni pamoja na kuendesha zoezi la waandishi kuchanga hili kuweze kusaidia kupata matibabu" Alisema Bi Mgoja
Kwa upande wake, mjomba wa Karume Salum Ahamad Idobelele amesema alianza kuangaika na Karume akiwa na miaka 16 baada ya kupata uvimbe huo na baadae kubahatika mwaka huu kukutana na waandishi wa habari kupitia Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam ambao walibeba jukumu la kumtafutia msaada wa matibabu kwa kumpeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke na kisha kupewa rufaa ya kuja Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Pichani Bw. Karume Karume (41) aliyesumbuliwa na uvimbe sehemu mbalimbali za mwili wake kwa zaidi ya miaka 25. Kabla na baada ya matibabu ambapo leo ameruhusiwa kwenda nyumbani baada ya kufanikiwa kufanyiwa upasuaji rekebishi na watalaam wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuondolewa uvimbe wenye uzito wa kilo tano.
No comments