Breaking News

TMA YAKUTANA NA SEKTA MBALAMBALI NCHINI ILI KUJIPANGA NA MSIMU WA MASIKA 2023

Dar es salaam; Tarehe 20 Februari, 2023
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na sekta mbalimbali nchini ili kujipanga na msimu wa masika, katika Ukumbi wa NIT, jijini Dar es salaam, tarehe 20 Februari, 2023.

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi, alisema lengo la mkutano huo ni kujadili mwenendo wa mvua za msimu wa Masika 2023 na kuandaa taarifa zinazolenga kuchochea matumizi sahihi za huduma za hali ya hewa kulingana na utabiri utakaotolewa. Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano na ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.

“Tunapoelekea kutoa utabiri wa mvua za Masika (Machi hadi Mei), 2023 ninapenda kuipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kuendelea kushirikisha wadau mbalimbali kutoa michango yao katika shughuli za utoaji wa huduma za hali ya hewa ambazo ni pamoja na mchakato wa utabiri wa misimu ya mvua. Ushirikiano na ushirikishwaji huu ni muhimu sana hasa katika kipindi hiki ambapo dunia pamoja na nchi yetu tunakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa”. Alisema Dkt. Nyenzi.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuchukua hatua thabiti za kukabiliana na hali hii kwa kuimarisha miundo mbinu ya Hali ya Hewa ikiwemo ununuzi wa vifaa kama vile vifaa vya kisasa vinavyojiendesha vyenyewe na Rada”. Alisisitiza Dkt. Nyenzi.

Awali wakati akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu, TMA, Dkt.Ladislaus Chang’a aliishukuru Serikali na wadau wa maendeleo kwa kuendelea na uwekezaji katika miundombinu ya hali ya hewa hapa nchini, kupitia jitihada hizo, Mamlaka imeendelea kutoa taarifa za utabiri wa maeneo madogo madogo kwa wilaya zote za mikoa iliyopo katika ukanda unaopata mvua za Masika na hivyo kusaidia  katika kufanya maamuzi stahiki kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi, na pia kupunguza madhara ya hali mbaya ya hewa inapojitokeza.

“Kama mnavyotambua, mvua za Masika ni mahsusi kwa maeneo ya pwani ya kaskazini, nyanda za juu kaskazini mashariki, na Ziwa Viktoria ambayo hupata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Masika na Vuli). Mvua hizi zina mchango mkubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishati, maji n.k. Hivyo, taarifa sahihi za hali ya hewa pamoja na athari zake ni muhimu kupatikana kwa wakati ili kuwezesha jamii na wadau kujipanga na kuandaa shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao ”. Alisema Dkt. Chang’a.

Kwa upande wake Bi,Wilfrida Ngowi Mratibu Kitengo cha Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu alisema ‘’Serikali imeweka na imeendele kuimarisha mifumo na taratibu ya kukabiliana na maafa yatokanayo na matukio ya Hali mbaya ya Hewa ikiwemo mafuriko.

Naye, James Kirahuka Mhandisi Rasilimali Maji, akiwasilisha mrejesho wa msimu wa mvua uliopita, alisema baada ya kupokea utabiri wa hali ya hewa kwa msimu wa mvua za Vuli 2022 ukionesha upungufu wa mvua, TANESCO ilijipanga kwa kuongeza njia zingine za uzalishaji wa umeme ili kupunguza makali ya changamoto ya upatikanaji wa umeme.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, inatarajia kutoa rasmi taarifa  ya msimu wa mvua za Masika tarehe 23 Februari 2023.








No comments