RUNGWE Aitaka Serikali Kuruhusu Vyama Vya Siasa Kufanya Mikutano Ya Siasa.
MWENYEKITI wa Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Hashim Rungwe, ameitaka Serikali kuruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa ikiwamo mikutano ya hadhara na maandamano.
Akizungumza Dar es Salaam, wakati wa mkutano mkuu wa chamahicho ambao pamoja na mambo mengine ulilenga kufanya uchaguzi wa kupata viongozi wapya watakaoongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
“Tunapeleka ujumbe Serikalini kwamba watufungulie tufanye siasa, waache kuzuia zuia hivi vyama siasa ndio maisha ya mwanadamu, binadamu anaishi kwa maneno sasa ukizuia wananchi wanakosa pa kusemea.
“Wakiwa na dukuduku zao wangesemea pale lakini sasa hawana pa kwenda kutolea hayo maneno kwa hiyo ni ujumbe wangu ninaoutuma kwenu kwamba serikali iweze kurekebisha haya mambo watu wafanye siasa kama ilivyokuwa hapo nyuma,” Rungwe.
Kuhusu uchaguzi huo wa jana Rungwe alisema viongozi waliokuwapo wamejitahidi kukifikisha chama hapo kilipo na kwamba watarudi madarakani ikiwa watachaguliwa na wanachama wa chama hicho.
“Kwa hiyo sisi kwa kusema kweli hatuna mengi, mimi ninawategemea wajumbe, nitagombea na wenzangu watagombea itajulikana baada ya uchaguzi kwamba nani ameshinda na nani hakushinda” alisema Rungwe.
Rungwe alisema ikiwa atachaguliwa ataendeleza mapambana na kuhakikisha demokrasia inapatikana ili wananchi wapate pa kutolea dukuduku zao kwa sababu wamebanwa kiasi cha kushindwa hata kufanya hata mikutano.
“Kama hivi hapa sisi tumekutana, Polisi walitakiwa waje kutulinda kama wao wana taarifa zozote kuwa kuna watu wanataka kuleta fujo sio kutuambia tuondoke.
“Chama chochote kinachotaka kufanya siasa kilindwe tukitaka kufanya siasa za barabarani tulindwe, tukitaka kufanya siasa za majukwaani tulindwe lakini siyo kutwambia acheni na wengine unawaambia waendelee na siasa. Hili lazima lirekebishwe limekaa vibaya” alisema Rungwe.
Alishauri klufanyiwa kazi sera ya njaa ambayo imekuwa ikinadiwa na chama hicho ili kuwezesha wananchi kupata chakula cha uhakika kabla ya kuwaambia mambo mengine ya kimaendeleo.
Rungwe alisema hata watoto wasipopata chakula hawawezi kuelewa kile wanachofundishwa shuleni, hivyo ni lazima kuhakikisha wananchi wanalima kilimo cha umwagiliaji na si cha kutegemea mvua za msimu.
Rungwe alisema pamoja na kujengwa kwa reli itakayokuwa ikisafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda nchi za Burundi na Rwanda itapendeza reli hiyo itatumika kusafirisha mazao ya chakula kwenda katika nchi hizo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chaumma Zanzibar, Mohammed Masoud Rashid alisema kufanyika kwa uchaguzi huo ni kutekeleza matakwa ya sheria ya vyama vya siasa nchini inayotaka vyama vya siasa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano. “Ni matumaini yetu kwamba tutafanikiwa ili tukienda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa tuwe tumemaliza,” alisema Bw Rashid. |
No comments