Breaking News

WAKUU WA MAJESHI EAC, SADC WAPEWA SIKU TANO

Dar es salaam - Wakuu wa Majeshi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wametakiwa kukutana ndani ya siku tano, ili kutoa mwongozo wa kiufundi juu ya usitishaji wa mapigano wa haraka na bila masharti katika mji wa Goma nchini DR Congo.

Kauli ya kuwataka wakuu hao wa majeshi kukutana imetolewa kupitia maazimio ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa EAC na SADC waliokutana Ikulu jijini Dar es Salaam kuzumzia mgogoro wa kivita unaondelea katika miji ya Mashariki ya DR Congo, ambapo taarifa zinasema zaidi ya watu 3,000 wamepoteza maisha hadi sasa.

Mkutano huo umehudhuriwa na Rais wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa EAC na Rais wa Kenya Dk William Ruto, Mwenyekiti wa SADC na Rais wa Zimbabwe Dk Emerson Mnangagwa, Raia wa Uganga Yoweri Museveni, Rais wa Rwanda Paul Kagame na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa.

Wengine ni Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema, Waziri Mkuu wa Burundi Gervas Ndirakobuca na mawaziri kutoka Malawi, Madagascar, Sudan Kusini, Angola na kwingineko.

Wakuu hao wa nchi za EAC na SADC wamesema wakuu wa majeshi wanapaswa kukutana ndani ya siku tano na kutoa miongozo ikiwemo utoaji wa misaada ya kibinadamu, kuandaa mpango wa usalama wa Goma na maeneo jirani, kufungua njia kuu za usambazaji, na kufungua Uwanja wa Ndege wa Goma mara moja.

Pamoja na viongozi hao wa SADC na EAC kutoa azimio dhidi ya wakuu wa majeshi pia wameazimia kuwa michakato ya Luanda na Nairobi iendelee kutekelezwa.

Pia viongozi hao wameazimia kusitishwa mapigano huko Mashariki ya DR Congo haraka iwezekanavyo.

Azimio lingine ni kurejesha huduma muhimu na njia za ugawaji wa chakula na bidhaa nyingine muhimu, ili kuhakikisha msaada wa kibinadamu unawafikia wahitaji.

"Kutafuta suluhisho la amani kwa mgogoro wa DRC kupitia michakato ya Luanda na Nairobi kwa kuunganishwa na kuimarishwa kuwa mchakato mmoja wa Luanda-Nairobi. Wawezeshaji wa ziada, wakiwemo kutoka nje ya kanda, wanapaswa kuzingatiwa na kuteuliwa,".

Azimio lingine ni kuanzishwa kwa mazungumzo ya moja kwa moja na majadiliano kati ya wadau wote wa serikali na wasio wa serikali, wa kijeshi na wasio wa kijeshi, wakiwemo M23, chini ya mfumo wa mchakato wa Nairobi-Luanda.

Viongozi hao pia waliazimia kuondolewa kwa kundi la FDLR na kuondolewa kwa hatua za ulinzi za Rwanda pamoja na kuondolewa kwa vikosi vyake kutoka DRC kama ilivyokubaliwa katika mchakato wa Luanda.

Pia wameazimia mkutano wa pamoja wa mawaziri wa EAC na SADC uitishwe ndani ya siku 30 ili kujadili ripoti ya mkutano wa pamoja wa wakuu wa majeshi (CDFs) kuhusu usitishaji wa mapigano na masuala mengine

Aidha, waliazimia kuwa mpango wa kuondoa vikosi vya kigeni ambavyo havijaalikwa kwenye ardhi ya DRC uandaliwe na kutekelezwa

Halikadhalika viongozi wa kanda wamethibitisha kutoa ushirikiano wa msaada wao kwa DRC katika kulinda uhuru wake na mipaka yake ya ardhi

Viongozi hao waliazimia Mkutano wa pamoja wa EAC na SADC ufanyike angalau mara moja kwa mwaka, pale inapohitajika.

Kupitia mkutano huo viongozi hao walimpongeza na kumshukuru Rais Samia kwa kukubali kuandaa mkutano huo ambao umetoka na maazimio ya kuikomboa DR Congo.

Pia waliwapongeza Rais Ruto na Mnangagwa kuongoza jumuiya zao katika kufanikisha mkutano huo muhimu kwa DR Congo na watu wake 

No comments