SERIKALI YA SWEDEN YAAHIDI KUENDELEZA USHIRIKIANO WA KIFEDHA KATIKA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UMEME NCHINI
Na. Agnes Njaala , Korogwe - Wawakilishi wa Serikali ya Jamhuri ya Sweden (Swedish International Development Corporation Agency ) ambao ni wadau wa maendeleo nchini Tanzania wameahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya umeme ili kuleta maendeleo yenye tija kwa wananchi na nchi kwa ujumla.
Ahadi hiyo imetolewa Februari 06, 2025 na msimamizi wa ufadhili upande wa Serikali ya Sweden wa mradi wa ukarabati wa Kituo cha Kufua Umeme cha Hale Bw. Stephen Mwakifamba wakati wa kikao cha mwaka cha tathimini ya utekelezaji wa mradi huo kilichofanyika kituoni hapo.
“Hatua iliyofikiwa ya ukarabati wa kituo hiki ni nzuri na inaridhisha hivyo tunaimani kuwa mradi utakamilika ndani ya muda uliopangwa, tunaishukuru Serikali ya Tanzania kushirikiana na Serikali ya Sweden kufikia hatua hiyo, tunaahidi kuuendeleza ushirikiano huu katika utekelezaji wa miradi mingine kama hii ” ameeleza Bw. Mwakifamba.
Amesema lengo kubwa la miradi kama hiyo ni kuongezea nguvu kwenye jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi wake na ukizingatia kwa upande wa Mradi huo wa Kituo cha Hale ni wa muda mrefu tangu miaka ya 1960 hivyo kufanya ukarabati wake kunahitaji nguvu ya ziada.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Dkt. Khatibu Kazungu anayeshughulikia masuala ya Umeme na Nishati Jadidifu amesema , Serikali ya Sweden imekuwa ni mdau muhimu sana katika kuchangia maendeleo ya ukarabati wa kituo hicho kwani wametoa zaidi ya Shilingi Bilioni 30 za kitanzania kwa ajili ya ukarabati huo.
“Serikali ya Sweden imekuwa ikifadhili miradi mingi sana ya umeme nchini kama vile Kihansi, Kidatu, Mtera, Pangani Falls na Hale , nichukue nafasi hii kwa niaba ya Uongozi wa Wizara ya Nishati kutoa shukrani za dhati kwa msaada wao mkubwa katika kuimarisha na kuendeleza miradi ya Sekta ya Nishati katika Taifa letu” ameeleza Dkt. Kazungu.
Aidha , amebainisha kuwa , Serikali iliyopo madarakani imekuwa na msaada mkubwa sana katika kuhakikisha inatoa fedha za kutosha ili miradi ya umeme iweze kukamilika kwa wakati huku ikishirikiana kwa karibu zaidi na wadau wa maendeleo.
Ukarabati wa Kituo cha Kufua Umeme Hale ulianza tangu mwezi Aprili mwaka jana ambapo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu 2025 ukihusisha mashine mbili zenye uwezo wa kuzalisha megawati 10.5 kila moja .
Kukamilika kwake kutaongeza uzalishaji wa umeme utakaochangia ongezeko la megawati 21 katika Gridi ya Umeme ya Taifa ya Tanzania na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme hususani katika Mikoa ya Kanda ya Kaskazini.
No comments