Sakata La Pasipoti Mpya Lazidi Kunoga......Uhamiaji Yawashukia Wanasiasa, Yawataka Wananchi Wawapuuze
IDARA ya uhamiaji
nchini imewataka watanzania kupuuza habari zinazozagaa kuhusu uvumi wa pasipoti
mpya kuwa zimechakachuliwa.
Kauli hiyo
imetolewa jana na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini, Dkt. Anna
Makakala jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema
wananchi wanatakiwa kupata taarifa sahihi kila mara juu ya kila jambo
linalohusu maendeleo yao na mambo yanayoletea ustawi wa Taifa , na kwamba wao
Idara ya Uhamiaji ndio wenye taarifa sahihi zinazohusu Mchakato mzima wa
Pasipoti Mpya za Kielektroniki
Hivi karibuni Rais
Dkt. John Magufuli wakati akizindua hati mpya za kusafiria alisema kumekuwapo
na wahujumu wa mchakato huo ambao hawakufanikiwa kuiba sh. bilioni 400.
Alisema kumekuwapo
na watu waliozunguka kila kona na kutumia kila njama zote kupiga vita mchakato
huo wakidhani watafanikiwa kuhujumu serikali.
Dkt. Anna Makakala
alisema hatua hizo za kutoa na kueneza taarifa zisizo sahihi zinawaletea
mkanganyiko wananchi na kudhoofisha mawazo na fikra chanya kwa Taifa lao
Alisema ni vyema
jamii ikatambua kuwa mchakato wa Pasipoti mpya ya kidigitali ni hatua kubwa kwa
Taifa hili na si vyema kuutolea Taarifa zisizo sahihi. Aliwasihi wanahabari
kupata taarifa kutoka katika vyanzo sahihi na kuzifikisha kwa walaji ambao ni
Wananchi.
Alisisitiza hatua
ya mafanikio ya matumizi ya hati hizo hazitarudi nyuma kwa sababu ya kuwapo na
taarifa zisizo sahihi zenye lengo la kupotosha ukweli wa mchakato huo.
“Ni vyema jamii kuelewa kazi ya hati hizo ni
kulinda usalama wa nchi yetu, hivyo Uhamiaji tutaendelea kudhibiti mipaka ya
Tanzania na kulinda usalama wa nchi kwa kuwezesha jamii na raia wa kigeni
kufuata taratibu katika utokaji,ukaaji na uingiaji wa kila mmoja,” alisema
Dkt. Makakala.
Alisema kila nchi
yenye kuhitaji maendeleo ni muhimu kutumia hati ya kusafiria ya kielektroniki
ili kufikia mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
“Mabadiliko ya
kidunia katika maendeleo yanatuonyesha wazi kuwa Taifa hili limefikia kuwa na
hati za kisayansi na kiteknolojia hivyo katika hati mpya,mtu yeyote hataweza
kutumia ujanja au kughushi na kutumika kwa matumizi yasiyo sahihi,” alisema
Dkt. Makakala.
Alisema anaamini
idara hiyo haitashindwa na wachache wanaokubali kutumika kuhujumu mchakato huo
kwa maslahi binafsi kwakuwa kushindwa kwa mchakato huo ni kupunguza hadhi ya
usalama wa nchi.
“Pasipoti ndio
kitu kinachotuwezesha kudhibiti wanaoingia nchini na kutoka, hiki ni
kitambulisho cha raia sehemu yoyote duniani wenye Pasipoti za Tanzania ni
mabalozi wa Tanzania.
"
Mfumo huu utawezesha kudhibiti ujanja wote unaotumika, kutakuwa na cheap na
security features nyingi. Sifa ya Taifa letu dunia imeharibika lazima kufanya
maamuzi kwa maslahi ya Taifa letu,” alisema.
Dk. Anna alisema
kufanikiwa kwa mradi huo wa e-Immigration kwa gharama ya dola za Marekani
milioni 57 imekuwa mwiba kwa vigogo walioondolewa Uhamiaji na sasa wanahaha kwa
aibu wakidai kwamba gharama iliyotajwa ni kwa ajili ya mradi mmoja tu wa
e-Pasipoti.
“Ni wajibu wa kila
mtanzania kuwa macho na wale wote wanaotumiwa na mafisadi kwa ajili ya
kuichafua serikali kwakuwa imezuia na kupambana na uhujumu uliotaka
kujitokeza,” alisema.
Alisema hati hizo
zitawezesha waliopotelewa na hati zao kutumia mfumo wa kiteknolojia na kupakua
app yake hata katika simu ya mkononi, hivyo kutambulika na kupewa msaada haraka
kokote duniani.
Alisema hati hiyo
inaviwango vyote vya ubora wa kimataifa pia itatumika kama kitambulisho kwa
nchi za Afrika Mashariki.
No comments