Bashe Awahenyesha Mawaziri Watano, Wakutana Kwa Dharura
Mawaziri watano jana walilazimika
kufanya kikao cha dharura bungeni baada ya uongozi wa Bunge kuagiza serikali
itoe majibu kutokana na hoja ya Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe.
Mawaziri waliokutana kutokana na hoja
hiyo ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,
Selemani Jafo; Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana
na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nishati,Dk. Medard Kalemani
na naibu mawaziri wa fedha, Dk. Ashatu Kijaji na wa maji, Jumaa Awesso.
Mbunge huyo aliwashtaki mawaziri
kwenye chombo hicho cha kutunga sheria akieleza kuwa wamekuwa chanzo cha mateso
na mahangaiko kwa wananchi wa Nzega.
Huku akitumia Kanuni ya 47 kuliomba
Bunge liahirishe shughuli zake za jana na kujadili jambo la dharura, Bashe
aliwataja hadharani Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, Waziri wa
Nishati, Dk. Medard Kalemani, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwelwe na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -Tamisemi, Selemani Jafo, ambao alidai wamesababisha
wananchi wa jimbo lake kukosa maji kwa siku ya 13 mfululilo hadi kufikia jana.
Alisema huduma hiyo haiko jimboni
kwake kwa kipindi hicho cha wiki mbili kutokana na mamlaka ya maji kukatiwa
umeme kutokana na serikali kutolipa malimbikizo ya madeni kwa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco).
Mbunge huyo alisema amekuwa
akiwasiliana na serikali lakini hakuna kinachoendelea na wahusika wamekaa kimya
ilhali wananchi wa jimbo lake hilo wanapata taabu.
“Ndugu zangu wabunge na hasa wabunge
wa CCM, naombeni mniunge mkono katika jambo hili. Nzega ni siku ya 13 sasa
hatuna maji, wanawake wanateseka bila maji na kunilazimu ninunue maji kwa ajili
ya hospitali,” alisema Bashe aliyeonekana kuzungumza kwa hisia kali.
Alibainisha kuwa yuko tayari kwa
jambo lolote kwa kuwa ni wananchi wake wanaoumizwa na serikali kwa kukatiwa
maji katika kosa ambalo serikali ndiyo mhusika mkuu wa deni hilo.
Alisema wananchi wake wanapata mateso
lakini serikali haijawahi kupeleka majibu ya aina yoyote kuhusu mateso hayo na
bado inaonekana kutojali licha ya Bunge kutaka mawaziri wakutane naye
kujadiliana.
"Waheshimiwa wabunge, naomba
tusaidiane katika kumsaidia Rais wetu, hali ni mbaya. Wapendwa leo ni Nzega,
lakini itakuwa kesho kwa mwingine, lolote litalotokea huko litakuwa juu ya
mawaziri hao,” alisema Bashe na kutoa hoja.
Kutokana na hoja hiyo, Mwenyekiti wa
Bunge, Andrew Chenge, aliyekuwa anaongoza kikao cha jana, alisimama na kueleza
ukubwa wa tatizo la maji kuwa ni la nchi nzima, hivyo halitakiwi kuupuzwa na
akaomba kuwatendea haki wananchi katika maeneo yote.
Kwa uzito huo, Chenge alimtaka Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu Wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama, kueleza hatua ambazo zimechukuliwa na serikali
kutatua changamoto hiyo.
Waziri huyo aliagiza mawaziri
wanaohusika na maji, nishati na fedha kukutana kwa dharura kwenye moja ya kumbi
za Bunge mara moja pamoja na Bashe baada ya kuahirishwa kwa shughuli za chombo
hicho jana mchana.
Kutokana na majibu hayo, wabunge
wengi walisimama na kuomba miongozi huku Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM),
akieleza kuwa tatizo la maji kuwa ni kubwa na hata katika wilaya yake ambako
watumishi walikula fedha za mradi wa maji lakini wakahamishwa na kuacha mradi
ukiwa haujakamilika.
Nje ya Bunge, Bashe alisema kuwa kikao baina yake na mawaziri hao kilifanyika kwa nusu saa kwenye moja ya kumbi ndogo zilizoko ndani ya jengo la Ukumbi wa Bunge na akabainisha kuwa katika kikao hicho waliazimia serikali iji-commit' kulipa deni la umeme na mamlaka ya maji irudishiwe huduma ya umeme haraka.
No comments