Breaking News

TMA NA EMEDO WAONGEZA NGUVU USAMBAZAJI WA TAAARIFA ZA HALI YA HEWA ZIWA VICTORIA

Dodoma - Katika kuendelea kuboresha usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetembelewa na Wataalamu wa Shirika lisilo la Kiserikali la Uhifadhi wa Mazingira na Maendeleo ya Kiuchumi la EMEDO ambalo linalojihusisha na uhifadhi wa mazingira katika maeneo yanayozunguka Ziwa Viktoria. 

Ziara ya EMEDO ilikuwa na lengo la kujadiliana namna ya kuendelea kushirikiana katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wa maeneo yanayozunguka Ziwa Viktoria hususani wavuvi. Kikao kati ya TMA na EMEDO kimefanyika Februari 4, 2025 kwenye Ofisi za TMA Makao Makuu, Jijini Dodoma.
Wakati wa ziara hiyo yamefanyika majaribio ya matumizi ya kifaa maalumu cha usambazaji wa taarifa za hali ya hali ya hewa “Electronic Weather Board”, ambacho kitawasaidia wavuvi na watumiaji wa Ziwa Victoria kwenye kisiwa cha Goziba kuona utabiri wa hali ya hewa unaotarajiwa katika Ziwa kwa lengo la kufanya maamuzi sahihi ili kuokoa maisha na mali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Ladislaus Chang'a aliushukuru uongozi wa Shirika la EMEDO kwa ushirikiano unaoendelea kati ya Taasisi hizi wenye lengo la kusambaza taarifa na elimu ya matumizi sahihi ya taarifa zitolewazo na TMA katika maeneo ya ziwa Victoria.
"Haya ni mambo muhimu sana tunapaswa kufanya ili kuoanisha shughuli zetu na maono ya kimkakati na kuleta thamani kwa kile tunachofanya. Nimevutiwa sana na ushirikiano huu kwa sababu tunataka kila mmoja wetu kuchangia katika kufikia maono ya Taifa. Kwa mfano, kuimarisha hatua za kijamii kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa Duniani ". Alisema Dkt.Ladislaus Chang'a 

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa EMEDO, Bi. Editrudith Lukanga, alishukuru pia Mamlaka kwa ushirikiano huu na kusema kuwa TMA imekuwa ikitoa wataalamu wake katika kutoa mafunzo kwa jamii na pia kutoa utabiri wa hali ya hewa, jambo ambalo limekuwa na manufaa kwa jamii.

No comments