Breaking News

RUNGWE: UKAWA wanaitega NEC uchaguzi Siha, Kinondoni.

Hashim Rungwe 

IMEBAINIKA kuwa ushiriki wa Chadema katika uchaguzi mdogo wa marudio wa ubunge katika jimbo la Kinondoni na Siha ni mtego uliowekwa na UKAWA kwa tume ya taifa ya uchaguzi (NEC )

Mtego huo ni UKAWA kujiridhisha kama NEC inauwezo wa kuwadhibiti wakuu wa wilaya kutoingilia mchakato mzima wa uchaguzi.

Katika mahojiano maalum na matukio360, jijini Dar es salaam, mwenyekiti wa chama cha Chauma, Hashim Rungwe amesema kilichofanywa na Chadema kinaungwa mkono na Ukawa na kwamba walitangaza kurejea kwenye uchaguzi iwapo malalamiko yao yatashughulikiwa na moja ya lalamiko lilikuwa ni  wakuu wa wilaya kuingilia uchaguzi.

"Hivyo katika hili NEC imetuhakikishia kulishughulikia na tayari wamewaandikia barua viongozi hao wa wilaya kuwataka kutojihusisha na uchaguzi Sasa tunataka kuona kama kweli wamerekebisha na hatuwezi kuona kama tupo nje ya mpambano na kama hawajarekebisha tutazidi kulalamika,” Alisema Rungwe 

Rungwe amesisitiza  walichofanya Chadema ni maamuzi ya Ukawa kwa kuwa wakati wakiteua wawakilishi wa majimbo ya Siha na Kinondoni vyama vingine vilikuwa na uwakilishi walioshiriki kuwapitisha.

Walioteuliwa kugombea katika majimbo hayo ni Salum Mwalimu Juma  Kinondoni  na Elvis Christopher Mosi jimbo la Siha.

Lakini kwa upande wake katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi, Danda Juju ameshangazwa na uamuzi huo na kwamba msimamo wa mwisho wa vyama vinavyounda Ukawa ni kutoshiriki uchaguzi bado upo pale pale.

“Najisikia vibaya sana kuzungumza juu ya suala hili, na kwa bahati mbaya waandishi wa habari wamekuwa wakiniulizia kuhusu hili, nimekuwa sitaki kulizungumzia na pengine kwako wewe wacha nisema hivi,”

“Labda kwa ufupi ni sema kwamba azimio tulilokuwepo nalo la mwisho la vyama vinavyounda Ukawa bado liko palepale na nilikuwa nazungumza na mwenyekiti wa kamati ya uongozi CUF juu ya hili, Chadema wamefanya hivyo kama Chadema,” amesema Juju.

Amesema anatarajia kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif kujadili na kujua kilichojili na kwamba pia watafanya juhudi za kukutana na Chadema ili kulijadili suala hilo kwa kina.

Juju  amesema wakati Chadema ikisimamisha wagombea bado  yale waliyoyadai na shinikizo waliloweka NEC hadi  sasa matokeo yake hayajaonekana.

Amesema kuweka wagombea siyo vibaya lakini ilitakiwa busara kutumika ili wakutane Ukawa kwa pamoja wazungumze ili kuwa na mwelekeo wa pamoja 

No comments