MHE MBOWE: UPINZANI NI WITO, NINGEKUWA NA ROHO NYEPESI NINGEKUWA NISHAKIMBIA
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjY9WeJ_D5zs1DAyo1HFAWKxL3pvazrFo4bPSx1bX-9f2c9fKBPlfmsSI9ui1mkCgJPBnw2474hr_EnPIZLuh8hOh-6d-U2rdcXNBsbEvtBZOohaLpI68tJ7I5x_3AoMsp1LlHvlJGpP0lR/s640/1.jpg)
Wakati diwani wa saba wa Chadema
akijiuzulu jana, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amesema hata yeye
kama angekuwa na moyo mwepesi na mpenda fedha, angekuwa ameshahama upinzani.
Mbowe alisema jana kwamba kuwa
kiongozi wa upinzani awe mbunge, diwani, au mwenyekiti wa mtaa, kunahitaji roho
ngumu na kwamba hiyo si kazi ya watu wenye kupenda fedha, bali ni ya maumivu,
kudhalilishwa, kunyimwa ushirikiano, kufungwa wakati wowote na kunahitaji
msimamo wa hali ya juu.
“Upinzani
ni wito, wenye roho nyepesi hawawezi, kama ningekuwa napenda fedha, nina roho
nyepesi, ningeshachukua hizo pesa na ningeshakimbia kabisa upinzani,” alisema.
Mbowe amesema hayo wakati chama hicho
kikipitia misukosuko ya madiwani wake wa Mkoa wa Arusha kukihama na jana
ilikuwa zamu ya Diwani wa Ambuleni, Arumeru, Japhet Jackson.
Diwani huyo aliwasilisha barua yake
ya kuhama Chadema kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Meru, Christopher
Kazeri jana mchana pia kama wenzake sita, akisema anamuunga mkono Rais John
Magufuli.
Diwani wa karibuni kujiuzulu wa
Ngobobo, Solomon Laizer pia wa wilaya hiyohiyo katika jimbo linaloongozwa na
Joshua Nassari wa Chadema.
Akizungumza kwa simu jana, Mbowe
ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema wanaowania nafasi za uongozi na viongozi wa
Chadema wanahitaji kuwa na msimamo wa hali ya juu.
“Mara
nyingi wanaowania nafasi kwa upande wa upinzani, ni wale waliokomaa, lakini
katika uchaguzi uliopita, chama kilichopata watu wengi ni Chadema. Kutokana na
mfumo huo wa kuwafungulia milango, wakaingia wengi, mbu, mende na mambo
mengine,” alisema.
Kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni alidai kwamba kuondoka kwa madiwani hao wa Chadema
kunasababishwa na baadhi ya watendaji wa Serikali hasa wakuu wa wilaya ambao
wanataka kumfurahisha Rais.
“Inashangaza
kuona wote wanaojiuzulu wanatoa kauli moja ya kumsifu Magufuli, ina maana
hawana sababu nyingine labda pengine Chadema kuna matatizo, sera zao mbovu,
kuna hiki na hiki hakijakaa sawa,”alisema.
Aliongeza kuwa juhudi za kuwarubuni
viongozi wa Chadema zipo katika majimbo yote ya Chadema na juhudi hizo zinapata
nguvu zaidi mahali ambako kuna mkuu wa wilaya dhaifu ambaye anatumia nguvu za
ziada.
Alisema wamebaini kuwa baadhi ya
wakuu wa wilaya ndiyo wanaotumiwa na wamewekwa kwa makusudi kwa ajili ya kuua
upinzani nchini.
“DC
anawahimiza wanachama na viongozi eti wapeleke barua za kujizulu kwake, kwa
sababu ana jeuri ya mamlaka. Kisheria hana mamlaka ya kupokea barua ya
kujiuzulu kwa mwanasiasa. Tumebaini hawa baadhi ya watendaji wanatumiwa na
kuahidiwa makubwa endapo watawadhibiti wapinzani,” alisema.
Alisema walipata tetesi za kujiuzulu
kwa madiwani hao lakini hawakutaka kuchukua uamuzi wa kuwafukuza kwani si
vizuri kuishi kwa tetesi lakini kwa kuwa wameamua kuondoka anawatakia kila
heri.
Alisema baadhi ya madiwani hao
walionekana kwenye vikao vya CCM na kusema mtu anayezidiwa akili na kudanganywa
kwa fedha hata akibaki katika chama hatakuwa na maana.
“Kuliko
kubaki na watu wengi wanaopenda fedha, wanaohadaiwa kwa rushwa, bora tubaki
watu wachache wenye maadili,” alisema.
Mbowe alisema, licha ya Serikali
kuudhofisha upinzani, chama hicho kinaamini kuwa safari yake ni kama ya treni
ya kwenda Kigoma ambayo wapo wanaopanda na wanaoshuka.
“Bado
tunavuna maelfu ya wana CCM, alianza Edwin Mtei, lakini sasa tunazungumzia
wanachama zaidi ya milioni sita. Muelewe kuwa upinzani haudhoofiki, bali
unakua,” alisema.
Alisema wale waliodhani watapata
ulaji kama wa fedha, ndiyo wanaokuwa wepesi kuondoka na kwenda kutafuta
wanachokitaka.
“Tuna
imani watabaki wachache wenye imani na nafasi za walioondoka zitachukuliwa na
wengine walio bora zaidi,” alisema.
Kuhusu kuswekwa rumande kwa saa 48
kwa amri za wakuu wa wilaya, Mbowe alisema sheria za kumuweka ndani kiongozi
zina masharti yake.
“Kuna
utaratibu wa kufanya.DC sio polisi, anaweza kuagiza polisi, kamkamateni fulani
kisha mumhoji na kisha afunguliwe mashtaka, lakini si kumuweka ndani kwa saa
48. Haya maagizo yote yanatolewa na ngazi za juu. Sisi sasa tunawashtaki hao
Ma-DC wote na hata mimi nimemshtaki DC wa Hai, kwa kuharibu miradi yangu,” alisema.
No comments