WAZIRI MKUU; MARUFUKU KUWATANGAZA HADHARANI WATUHUMIWA WA DAWA ZA KULEVYA KABLA YA KUWACHUNGUZA KWANZA
Wakati
Serikali ikiendelea kujipanga kwa vita dhidi ya dawa za kulevya, Waziri Mkuu
Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa na wilaya kutotangaza majina ya
watuhumiwa kabla ya kufanyika uchunguzi na kujiridhisha.
Kauli
hiyo imekuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
kulaumiwa na watu tofauti kwa kitendo chake cha kutangaza majina ya watu
aliotaka kufanya nao mahojiano kuhusu matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Wengi
waliokosoa kitendo hicho, hasa wabunge, walisema kutangaza majina ni kuharibu
uchunguzi na pia kunachafua watu kabla ya kuthibitika kuwa wanajihusisha na
dawa hizo na kwamba chombo pekee kinachoweza kumtia mtu hatiani ni mahakama.
Watu
walioitwa kituo cha polisi jijini Dar es Salaam, wakiwemo wanasiasa, wafanyabiashara
wakubwa, viongozi wa dini na wasanii walihojiwa na baadhi kupekuliwa majumbani
na ofisini kwao kabla ya kwenda kupimwa.
Baadhi
ya watuhumiwa hao ni kiongozi wa kanisa
la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe, mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji na msanii nyota wa filamu,
Wema Sepetu.
Akizindua
Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya uliofanyika ofisi ya waziri Mkuu
jana, Majaliwa alisema wakuu wa mikoa wana nafasi nzuri ya kushiriki katika
vita hiyo kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu.
“Wakuu
wa mikoa mna kazi kubwa katika vita hii. Mkiwa wenyeviti wa kamati za ulinzi na
usalama, mpo kwenye nafasi nzuri ya kuendesha vita hii kwa mujibu wa sheria,
kanuni na taratibu,” alisema Waziri Mkuu mbele ya mawaziri ambao ni wajumbe wa
Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya na wakuu wa mikoa.
“Jiepusheni
kuwatangaza watuhumiwa kabla hatujafanya uchunguzi. Itakapotokea uchunguzi
umekamilika na kuwakamata watuhumiwa, msisite kuwatangaza kwenye vyombo vya
habari, msiogope. Serikali inawategemea na itaendelea kuwaunga mkono,” alisema.
Pamoja
na hayo, Majaliwa alisema Serikali haitawavumilia watendaji wa mamlaka
watakaochukua rushwa kwa lengo la kuwasaidia wahusika wa dawa za kulevya.
Alisema
anafahamu kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya ni vita kubwa na hilo
linatokana na kuhusisha wafanyabiashara wakubwa na watu maarufu.
“Watendaji
wa mamlaka kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kufahamu kuwa mmeaminiwa, hivyo
muwe waadilifu kwani mmekabidhiwa makubwa yanayohitaji uangalifu wa hali ya
juu,” alisema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria
kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya udhibiti wa dawa hizo nchini na hilo
litafanyika bila uonevu wala upendeleo.
“Dawa
za kulevya ni tatizo kubwa. Tanzania imekuwa ikitumika kama njia ya kupitishia
dawa hizo, hivyo mapambano yanapaswa kufanyika kwa nguvu kubwa. Sheria ya
udhibiti isimamiwe kikamilifu; masharti yote yaliyotajwa yatekelezwe bila
kumuonea mtu,” alisema Majaliwa ambaye kwa nafasi yake anakuwa mwenyekiti wa
baraza hilo.
Alisema
baraza hilo lina wajibu wa kusimamia utekelezaji wa sera ya udhibiti wa dawa za
kulevya nchini.
“Jukumu
hili ni kubwa. Sisi kama wajumbe wa baraza tunatakiwa kulitekeleza kwa uadilifu
na umahiri mkubwa. Sina shaka na wajumbe,” alisema.
No comments