SAKATA LA KUTIMUA WATANZANIA NCHINI MSUMBIJI, MWANAMKE ASIMULIA ALIVYOBAKWA NA ASKARI MSUMBIJI
Wakati
Serikali ikiahidi kufanya uchunguzi wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za
binadamu katika kutimua Watanzania nchini Msumbiji, mwanamke mmoja amesema
alibakwa na askari watatu kabla ya kuwekwa mahabausu ambako alikaa siku tatu
bila kula.
Mwanamke
huyo, aliyejitambulisha kwa jina la Halima (si jina lake halisi) ni mmoja kati
ya zaidi ya Watanzania 180 ambao wamekuwa wakitimuliwa nchini Msumbiji tangu
mwanzoni mwa wiki na wengi wakidai wana hati halali za kuishi nchi hiyo jirani
na wengine kulalamikia vitendo vya ukiukwaji haki wakati wa utekelezaji wa
operesheni hiyo.
Tayari
Serikali imesema kuwa itafanya uchunguzi wa madai hayo, ambayo yanaweza
kuharibu uhusiano wa muda mrefu wa Tanzania na Msumbiji.
Halima
anasema walianza kufukuzwa usiku wa Jumamosi ya Februari 11, muda ambao askari
hao waliutumia kumfanyia kitendo hicho.
Halima
anasema kuwa alisikia watu wakivunja geti la nyumba waliyokuwa wakiishi na
kudhania ni majambazi, kumbe walikuwa ni askari ambao waliwalazimisha kutoa
nyaraka zao zote za kuishi Msumbiji pamoja na pesa.
“Niliwasikia
wakivunja geti nikamwambia mume wangu watakuwa ni majambazi kumbe askari, mume
wangu akajificha chini ya uvungu, lakini wakamtoa na baadaye kututoa ndani na
kuanza kutupiga.”
Anasema
baada ya kipigo walilazimishwa kuzoa mali zao kutoka ndani na zikawekwa kwenye
gari la polisi na kisha kuwafunga mikono na baadaye kuwapeleka mahabusu.
“Cha
kushangaza tulibebeshwa vitu wenyewe kuweka kwenye gari pasipo kuelezwa sababu
baada ya hapo askari akanivuta nyuma ya nyumba na kuniingilia kimwili. Nikajua
ni mmoja, lakini waliendelea hadi wakafikia watatu,” alisema.
“Ninaona
aibu walinibaka kwa njia ya kawaida tofauti na taarifa za wengine wanaosema
tulibakwa kinyume na maumbile, si kweli. Nawaomba waelewe hatukubakwa kinyume
na maumbile kama wanavyosema ilikuwa kawaida.”
Hata
hivyo anaeleza baada ya hapo waliwekwa mahabusu kwa siku tatu pasipo kula, hali
iliyowalazimu kunywa maji yaliyokuwa yamewekwa chooni.
“Tulikaa
mahabusu siku tatu, hamna kula wala kunywa, chooni tulienda kwa mtutu
tukalazimika kunywa maji ya chooni kwa sababu hakukuwa na jinsi na njaa
ilizidi. Kwa hiyo inabidi useme unakwenda chooni ili ukanywe maji,” alisema
Halima.
Kutokana
na hali hiyo, Halima anashangazwa na kauli ya Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Dk
Susan Kolimba kwamba waliorudishwa hawakuwa na nyaraka huku kaimu balozi wa
Tanzania nchini Msumbiji akiwatangazia wengine kuondoka ndani ya siku tano.
“Kweli
mtu utathubutu vipi kuishi nchi ya watu bila kibali? Hata kaimu balozi na yeye
anatukana, kwamba hatujaingia na documents (nyaraka)? Ilibidi atutetee lakini
katukana. Mungu atatulipia,” alisema.
Mwanamke
mwingine aliyewekwa mahabusu kabla ya kurudishwa nchini, Mary Makundi anasema
askari wa kiume walimwambia awape fedha na alipowajibu kuwa hana, walimpekua na
kuzikuta.
Anasema
walizichukua fedha hizo pamoja na simu kabla ya kumpiga na kutaka kumbaka.
“Walivunja
mlango wakanikuta. Wakaniambia niwape nyaraka zangu. Nikawapa nikijua
wanazikagua tu na kuniacha, lakini cha kushangaza walizichana mbele yangu na
kunitaka niwape pesa na simu. Nikawaambia sina wakanipiga na kunikagua hadi
sehemu za siri na kuchukua pesa na simu,” alisema Mary.
“Baada
ya hapo walinipiga kwanza kabla ya kunifunga mkono. Askari mmoja akataka
kunibaka, nikamwambia kuwa hata kama hawatutaki nchini kwao, hawawezi
kuniingilia bila kinga.
“Nilipoona
hali imekuwa mbaya, nilisema wacha nigombane nife kwa silaha, lakini si
kubakwa.”
Mtanzania
mwingine Mohamedi Said ni mmoja wa wafanyabiashara walioambiwa waondoke pasipo
kuchukua chochote na anadai kuacha mali zake zote pamoja na nyumba aliyojenga.
“Polisi
walikuja ghafla wakatuambia wageni wote tunatakiwa tuondoke. Hapa nina vibali
vyote mpaka leseni ya biashara, lakini imebidi niondoke kwa sababu ya usalama
wangu,” alisema Said.
“Hakuna
anayejua sababu mpaka sasa. Nimekuja nyumbani kufuatilia haki yangu kwa sababu
mpaka kibali cha kujengea ninacho.
“Mpaka
sasa amekuja kaimu balozi kutoka ubalozi wa Tanzania na amesema kwa ripoti
aliyopewa ametupa siku tano tuondoke. Hatujui kwanini siku tano. Utahamishaje
vitu kwa siku tano au kumtafuta mnunuzi wa nyumba kwa siku tano kwa sababu
imenibidi niache duka kubwa na gari,” alisema Said.
Akizungumzia
tukio hilo, mwenyekiti wa Kijiji cha Kilambo kilichopo mpakani na Msumbiji,
Mohamed Mkama alisema wananchi wa kijiji chake wamekuwa wakishirikiana na wanakijiji
wa vijiji jirani vya Msumbiji, lakini tukio hilo limewashangaza.
Amesema
mara nyingi wamekuwa wakitembeleana na hata wengine kutoka upande wa Msumbiji
kuja kutibiwa Tanzania kutokana na ujirani mwema uliopo.
“Kijiji
changu kina vitongoji vitano ambavyo tumekuwa tukishirikiana na kijiji cha
upande wa pili kwa muda mrefu na wengine wana vitambulisho vya uraia mwema,
lakini tunashangaa kwanini wanarudishwa pasipo kuelezwa sababu,” alisema Mkama.
Ofisa
uhamiaji Mkoa wa Mtwara, Rose Mhagama alisema idadi ya Watanzania waliorudi na
kusajiliwa katika mpaka wa Kilambo ni watu 221 hadi kufikia jana mchana.
No comments