MFANYABIASHARA MANJI ALAZWA TENA TAASISI YA MOYO YA JAKAYA KIKWETE
Baada ya kupata dhamana ya Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu juzi, mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, amelazwa tena kwenye
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyoko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa
mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na Ofisa Uhusiano wa Taasisi hiyo jana,
Anna Nkinda, Manji alifikishwa hospitalini hapo juzi jioni ikiwa ni muda mfupi
baada ya kupata dhamana dhidi ya kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya heroin
inayomkabili.
“Ni
kweli Manji yupo hapa, aliletwa jana jioni (juzi) kwa matibabu ambapo hadi leo
(jana) ninavyoongea na wewe bado yupo hapa amelazwa anaendelea na matibabu kama
kawaida,” alisema Anna.
Hii
ni mara ya pili kwa Manji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu, kulazwa
kwenye taasisi hiyo.
Mara
ya kwanza ilikuwa ni Februari 12, mwaka huu alipolazwa hapo akitokea katika
Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, alipokuwa ameshikiliwa tangu Februari
tisa akifanyiwa mahojiano.
Mfanyabiashara
huyo alifika mwenyewe kwenye kituo hicho cha polisi kutokana na wito uliotolewa
na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyetaja majina 65 ya watu
aliodai wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
Mbali
na Manji, baadhi ya watu wengine waliotajwa na Makonda na kutakiwa kufika
kituoni hapo ni Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima,
Mbunge wa zamani wa Kinondoni, Idd Azzan ambao tayari wamehojiwa polisi huku
Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, akiwa bado hajahojiwa licha ya kutajwa kwenye orodha
hiyo.
Juzi
Alhamisi, Manji alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo
shauri lake lilisikilizwa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Cyprian Mkeha.
Karani
wa mahakama hiyo, Sarah Mulokozi, alimsomea mshtakiwa shtaka lake ambapo alidai
kuwa kati ya Februari 6 na 9, mwaka huu eneo la Upanga Sea View jijini Dar es
Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.
Mtuhumiwa
huyo alikana shtaka hilo na Mkurugenzi wa Mashtaka Msaidizi (ADPP), Osward
Tibabyekomya, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba
Mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.
Upande
wa mawakili wa utetezi ambao ni Alex Mgongolwa na Hudson Ndusyepo, waliiomba
Mahakama kumpa mshtakiwa dhamana kwa
sababu ya mashtaka yanayomkabili yanadhaminika.
Hakimu
Mkeha alisema mshtakiwa atakuwa nje kwa dhamana kwa kutakiwa kusaini hati ya
dhamana ya Sh milioni 10 pamoja na mdhamini mmoja wa kuaminika ambapo Katibu
Mkuu wa Klabu ya Yanga, Charles Mkwasa, alimdhamini Manji, ambaye aliachiwa kwa
dhamana hadi Machi 16.
Mara
baada ya kupata dhamana, Manji aliondoka mahakamani hapo saa 9:40 akiwa kwenye
gari yenye namba T670 BBX aina ya Hummer.
No comments