SERIKALI YAJIPANGA KUPIGA MARUFUKU UVUTAJI SIGARA HADHARANI
Wizara
ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ipo katika hatua za mwisho
za kutayarisha mwongozo wa kupiga marufuku matumizi ya uvutaji wa sigara
hadharani ili kudhibiti maradhi yasiyoambukiza yanayotokana na sigara.
Hayo
yalisemwa na Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu
uvutaji wa sigara hadharani katika sehemu za mkusanyiko na kusababisha usumbufu
mkubwa kwa wananchi.
Alisema
tayari Wizara ya Afya imewasilisha muswada wa kulinda afya ya jamii ambao moja
ya kazi yake kubwa ni kupambana na matumizi ya sigara katika jamii na sehemu za
mkusanyiko.
Akifafanua
zaidi, alisema utafiti uliofanywa kuhusu maradhi yasiyoambukiza unaonesha
kwamba upo kwa asilimia 38 ambayo yanahusishwa na uvutaji wa sigara.
Kombo
alisema mwongozo huo ukikamilika utaletwa mbele ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
na wajumbe kutoa maoni yao kabla ya kufanya kazi na kuwa sheria inayotakiwa
kutekelezwa na kusimamiwa.
Alisema
yapo matumizi mabaya ya uvutaji wa sigara hadharani ikiwemo sehemu za
mikusanyiko ya watu kama hospitalini na sehemu za kusubiri usafiri wa abiria na
kusababisha madhara makubwa ambayo hayaonekani kwa mara moja.
No comments