Breaking News

ACT WAZALENDO YATAJA MAADHIMIO SABA YA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025

Katibu mkuu wa chama cha ACT WAZALENDO, Ado Shaibu ametangaza maadhimio saba ya kikao cha halmashauri kuu kilichokaa February 23, 2025 jijini Dar es salaam.

Akisoma maadhimio hayo  amesema Kikao ambacho pia kilipokea na kujadili Taarifa ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, Hali ya Kisiasa Nchini na Mwelekeo wa Chama katika Kukabiliana na Mazingira mabovu ya Chaguzi nchini ambapo wajumbe kwa kauli moja waliadhimia kuwa kipaumbele cha Chama kwa sasa ni kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini utakaohakikisha HAKI na kuheshimiwa maamuzi na matakwa ya wananchi.

"Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo ilikutana kwenye kikao chake cha kawaida jana Kikao hicho kilipokea na kujadili Taarifa ya Uvurugaji wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, Hali ya Kisiasa Nchini na Mwelekeo wa Chama katika Kukabiliana na Mazingira mabovu ya Chaguzi nchini". Alisema Bw. Shaibu.

Alisema Halmashauri Kuu pia imejiridhisha kuwa maridhiano yaliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan yamesambaratika pamoja na falsafa yake ya 4R iliyokuwa inatumika kuvileta pamoja vyama vya upinzani na wadau wengine wa demokrasia nchini walimuunga mkono Rais Samia kutokana na ahadi yake ya kuboresha mazingira ya kisiasa nchini, kuhakikisha chaguzi zinakuwa huru za haki na za kuaminika. Halmashauri Kuu imejiridhisha kuwa hakukuwa na utashi wa kisiasa kutekeleza ahadi hii. 

Hivyo basi, Halmashauri Kuu inamtaka Rais Samia kujitathmini juu ya tofauti iliopo baina ya ahadi anazotoa kwa maneno na kukosekana kwa vitendo katika kutekeleza ahadi hizo. 

Ametaja maadhimio mengine kuwa ni Chama kimetakiwa kifanya uchambuzi na kuandaa ripoti ya kina juu ya vitendo vya uvunjifu wa haki za binadamu nchini vilivyofanywa na vinavyoendelea kufanywa na Serikali za Chama cha Mapinduzi (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar) yakiwemo matukio ya mauaji na utekaji na madhila ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024. 

Ambapo kwa upande wa Zanzibar, chama tayali kinayo ripoti ya kina juu ya mauaji ya raia 21 na matukio mengine ya ukatili wa kutisha yaliyofanyika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2020 na vitendo vyote vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu Zanzibar tangu mwaka 2020-2025. 

"Halmashauri Kuu imeelekeza Ripoti hizo zichapishwe na kupelekwa kwa wadau wa demokrasia nchini pamoja na jumuiya ya kimataifa ikiwemo taasisi za fedha za kimataifa na pia kushirikiana na taasisi hizo kufikisha kesi katika Mahakama za Kimataifa". Alisema Bw. Shaibu

Katika hatua nyingine Halmashauri Kuu imekitaka Chama kuendeleza ushirikiano na vyama vingine makini vya upinzani na wadau muhimu wa demokrasia ikiwemo Asasi za Kiraia na viongozi wa dini katika kujenga vuguvugu la kitaifa la kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini. 
 
Aidha ametaja maadhimio mengie kuwa ni Chama kiandae operesheni kubwa ya kulinda demokrasia nchini Tanzania itakayojulikana kama OPERESHENI LINDA DEMOKRASIA ambapo Lengo la operesheni hiyo ni kuhamasisha umma wa Watanzania kupigania haki zao na kutokubali kuwa wanyonge. 
 
Aidha halmashauri Kuu pia imekitaka Chama kijikite katika kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini ikiwemo kufanyika kwa mabadiliko madogo ya katiba (minimum constitutional reforms), kuundwa kwa Tume Huru za Uchaguzi (NEC na ZEC kwa upande wa Zanzibar) na kupinga kwa nguvu zote kura ya mapema kwa upande wa Zanzibar. 
 

No comments