Breaking News

CHAMA CHA NLD CHAJIWEKA MGUU SAWA NA UCHAGUZI MKUU

Dar es salaam - Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD) Mhe. Doyo Hassan Doyo, alielezea hatua mbaimbali zinazochukuliwa na chama hicho kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Akizungumza na baadhi ya vyombo vya habari Makao Makuu ya chama hicho, amesema chama hicho kimeanza kufanya vikao mbalimbali vya tathmini ya Uchaguzi uliopita, hususan Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji, na vitongoji, huku lengo kuu likiwa ni kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu. Aliongeza kuwa tathmini hiyo inalenga kubaini namna chama hicho kitakavyoshiriki katika uchaguzi huo mkubwa na kuhakikisha kuwa hakikosi nafasi yake katika ulingo wa siasa.

Pamoja na kukutana na changamoto katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vijiji, na vitongoji, Katibu Mkuu wa NLD alisisitiza kuwa hilo halitakuwa kikwazo kwa chama hicho kushiriki katika Uchaguzi Mkuu. Alisema, "Kwa wale ambao wana sababu za kususa, na wasuse, lakini Chama cha National League for Democracy (NLD) hakiwezi kumuachia nguruwe shamba la miogoo. NLD tutashiriki uchaguzi mkuu kwa kiwango kile kile mpaka dunia ijuwe kwamba haki yetu inapokonywa hapa."

Chama cha NLD kimeendelea na vikao vya kikanuni, lengo likiwa ni kupata wagombea wanaokubalika katika jamii kwa ajili ya nafasi za Ubunge, Urais, na Udiwani. Maandalizi ya chama hicho yanaendelea kwa kasi huku viongozi wakiwa na dhamira ya kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Oktoba mwaka huu unakuwa na uwakilishi bora kutoka NLD.

No comments