WAZIRI KOMBO AKUTANA NA WABUNGE WA HUNGARY
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Wabunge wa Bunge la Hungary wanaounda Chama Rafiki cha Ushirikiano wa Kibunge kati ya Bunge la Tanzania na Bunge la Hungary.
Wabunge hao wa Hungary wakiongozwa na Mwenyekiti mwenza wa Chama hicho Bi. Mónika Bartos,wamekutana na Mhe. Waziri na Ujumbe wake katika moja ya Ukumbi wa Mikutano katika Bunge la Hungary.
Katika mazungumzo yao Mhe Waziri Kombo na Wabunge hao wamekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa Kibunge ‘Parliamentary Diplomacy’ kwa kuwa na ziara za viongozi wa mabunge na wabunge ili kubadilishana uzoefu, ujuzi na utalaam kuhusu masuala ya Bunge.
Maeneo mengine waliyokubaliana ni pamoja na kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Hungary kupitia sekta za kipaumbele za elimu, afya, utamaduni, michezo, afya, kilimo, biashara, uwekezaji, usambazaji maji, mazingira, mabadiliko ya tabianchi, na viwanda.
Mhe. Waziri Kombo pia amewakaribisha Wabunge hao kutenbelea Tanzania ili kujionea jitihada zinazofanywa na Serikali katika maeneo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi kupitia programu mbalimbali kama nishati safi ya kupikia.
Ameongeza kuwa ziara hiyo itatoa fursa ya kukutana na viongozi wa Bunge la Tanzania na viongozi wengine ili kujadili maeneo muhimu ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Hungary.
No comments