MBUNGE MAVUNDE AKABIDHI NYUMBA KWA WATOTO WALIOANGUKIWA NA NYUMBA JIJINI DODOMA
Mbabala, Dodoma - Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde leo amekabidhi nyumba kwa watoto Baraka Ijinji na Hamis Ijinji wa Mtaa wa Nguji,Mbabala Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya kuwajengea nyumba kufuatia kubomoka kwa nyumba yao ya awali iliyopelekea kifo cha Mama mzazi wa watoto hao.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo mbele ya uongozi wa Kata na kusindikizwa na dua na maombi yalioongozwa na Viongozi wa Dini.
“Mtakumbuka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa mfulululizo wa miaka miwili imepelekea maafa makubwa ya kuharibu mali na kupoteza maisha ya baadhi ya wananchi.
Watoto hawa Hamis na Baraka walipatwa na kadhia hiyo ya kudondokewa na nyumba ambayo ilipoteza maisha ya mama yao na wao kuokolewa na wasamaria wema.
Niliahidi kuwajengea nyumba watoto hawa ili kuwasaidia kupata makazi yao ya kudumu,namshukuru Mungu leo nimekamilisha ahadi yangu na nimekabidhi nyumba hiyo.
Aidha nitaendelea kuwasimamia kwa mahitaji yao muhimu kwa kadri Mungu atakavyoisaidia”Alisema Mavunde.
Akishukuru kwa niaba,Mlezi wa watoto hao Mchungaji Lazaro Peter amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kutimiza ahadi na kuwafariji watoto hao kwa kuwaboreshea makazi na kuahidi kuendelea kuwasimamia watoto hao katika malezi bora ili watimize ndoto zao
Naye Diwani wa Kata ya Mbabala Mh. Paskazia Mayala amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kuwa karibu na kuwajali watu wenye mahitaji kama alivyofanya kwa watoto na kumuomba kuendelea kuwagusa watu wenye mahitaji kadri Mwenyezi Mungu atakavyomjaalia.
No comments