Breaking News

MWENYEKITI WA BODI YA WAKURUGENZI NCAA AIPONGEZA SUMA JKT

Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kupitia SUMA-JKT kutokana na kazi kubwa wanayoifanya katika ujenzi wa nyumba 2,559 katika kijiji cha Msomera Wilayani Handeni mkoani Tanga.

Akizungumza kwa niaba ya wakurugenzi wa bodi wa Mamlaka hiyo  mara baada ya bodi hiyo kumaliza ziara yao ya kikazi katika kijiji hicho Jenerali Venance Mabeyo (Mstaafu) amesema kuwa kazi kubwa inayofanywa na jeshi katika ujenzi huo ni lazima iungwe mkono na wadau wengine wa kisekta ili kukamilisha zoezi hilo haraka ili wananchi waliojiandikisha kwa hiari kutoka ngorongoro waendelee kuhamia.

Amesema katika ziara hiyo bodi yake imejionea kusuasua kwa baadhi ya sekta katika utekelezaji wa majukumu yao hivyo kushauri kila mdau ni muhimu kuhakikisha anatekeleza majukumu yake.

“Jeshi mnafanya kazi kubwa ni muhimu sana kila mmoja wetu atimize wajibu wake ili tuimarishe miundo mbinu ya kijiji hiki  hasa nyumba ili wananchi waweze kuhamia kutoka ndani ya hifadhi ya Ngorongoro,”aliongeza  mwenyekiti huyo.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Richard Kiiza amesema hamasa ya wananchi kuhamia katika kijiji hicho ni kubwa ambapo mamlaka itaendelea kuwahamisha kadri wanavyojiandikidha.

Kaimu Operesheni Kamanda wa mradi huo Luteni kanali Edward Mwanga aliwahakikishia wakurugenzi hao wa bodi kuwa ujenzi wa nyumba hizo utakamilika kutokana na kasi na ari ambayo wanayo katika utekelezaji.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Handeni mhe. Albert Msando amesema wataendelea kuwapokea wananchi wanaotoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kutimiza azma ya serikali ya kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na maisha bora.







No comments