JWTZ YAPELEKA VIJANA 5000 KUJENGA NYUMBA MSOMERA, KITWAI NA SAUNYI
Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea maneo ya Ngorongoro na Msomera kujionea hali halisi ya zoezi la kuhamisha wananchi.
Msomera, Tanga
Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi amesema Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limepeleka vijana kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 5000 katika maeneo ya Msomera, Kitwai na Saunyi.
Matinyi amebainisha hayo leo Januari 17, 2024 akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea maneo ya Ngorongoro na Msomera kujionea hali halisi ya zoezi la kuhamisha wananchi ambapo kwa Msomera pekee zitajengwa nyumba 2,559.
"Shukrani za juhudi zote zinazofanyika katika eneo hili la Msomera, zinaelekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiyo aliyeidhinisha pori hili la akiba kujengwa makazi mapya," amesema Matinyi.
Matinyi amesema kuwa Katika eneo hilo, zimepangwa zijengwe barabara zenye urefu wa KM 800 ambapo mpaka sasa KM 150 zimekamilika huku mpaka sasa jumla ya visima 10 vikiwa vimeshachimbwa na vingine vinaendelea kuchimbwa na umeme umeanza kusambazwa.
Kwamba Shule ya Msingi imeshakamilika huku Shule ya Sekondari ya kisasa yenye maabara za masomo ya sayansi, TEHAMA na maktaba, Zahanati, Kituo cha Polisi vikiendelea kujengwa.
Amebainisha kuwa katika eneo hilo Mnada umeshajengwa, malisho ya mifugo yameshapimwa na vituo vya kuuzia maziwa vinaendelea kujengwa.
Sambamba na hilo amesema Mawasiliano tayari yameshafikishwa na hatua inayofuata ni Mfuko wa Mawasiliano Tanzania kuendelea na usambazaji wa minara ya mawasiliano kwa kushirikiana na kampuni binafsi za simu. Vile vile amebeinisha kuwa Majosho yanaendelea kujengwa huku upimaji wa viwanja unaendelea.
Amesema katika awamu ya pili, kufikia Januari 12, 2024, kaya zilizojiandikisha kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro ni 525, kati ya kaya hizo, 126 zenye watu 812 na mifugo 2,581 tayari zimeshahama.
Kwamba Kaya zilizohama zimegawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza lenye kaya 74 lenye watu 520 na mifugo 1,599 limekuja Msomera na kundi la pili la kaya 52 lenye watu 292 na mifugo 982 wamechagua kwenda kwenye mikoa mbalimbali.
"Kwa ujumla wake, mpaka sasa kaya 677 zimeshahama kwa hiari kutoka Ngorongoro zikiwa na watu 3,822 na mifugo 18,102. Zoezi la uhamaji kwa hiari linaendelea, Januari 18, 2024, kutakuwa na kundi lingine la kaya 72 lenye watu 515 ambalo litaondoka Ngorongoro. Ujenzi wa nyumba 1,000 uko katika hatua mbalimbali za ukamilikaji wake," ameeleza Matinyi.
Matinyi amesema uondokaji wa wananchi kutoka Ngorongoro kwenda Msomera kutasaidia eneo la Ngorongoro kuondoa tatizo la mmomonyoko wa ardhi na uchafuzi wa aina ya mimea pamoja na kuondoa tatizo la magonjwa ya wanyamapori kuingiliana na mifugo.
"Nawashauri wote wenye mashaka na zoezi la kuhamisha watu kutoka Ngorongoro waje wauone ukweli na baada ya hapo wenye nia njema watasema ukweli. Serikali ina nia njema, hakuna muda ambao itakaa chini kwa ajili ya kufanya maamuzi yatakayoumiza wananchi wake," ameeleza Matinyi.
Post Comment
No comments