UJUMBE WA TANZANIA, MJI WA JINHUA WAJADILIANA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI
Ujumbe wa Wizara ya Madini na wadau uliopo nchini China ukiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo, Agosti 16, 2023 ulitembelea na kukutana na uongozi wa juu Mji wa Dongyang na wafanyabiashara wenye viwanda vikubwa ambapo walipata nafasi ya kujadiliana namna ya kutumia fursa ya uwekezaji katika Sekta ya Madini pamoja na namna ya kupata Soko la Madini ya Shaba kutoka Tanzania.
Katika hatua nyingine, ujumbe huo ulifanya mazungumzo ya ana kwa ana (Round Table Meeting) na wafanyabishara wa China pamoja na mamlaka mbalimbali zinazosimamia shughuli za kiuchumi za Mji wa Jinhua nchini humo wakiongozwa na Msaidizi wa Meya wa Mji wa Jinhua.
Lengo la mazungumzo hayo lilikuwa ni kujadili fursa za kiuchumi baina ya Tanzania na China kupitia Sekta ya Madini lakini pia kuanzisha uhusiano wa kiuchumi na Mji wa Jinhua sambamba na kuendelea kudumisha uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu baina ya Tanzania na China.
Ujumbe huo wa wadau wa Sekta ya Madini wapatao 100 wakiwemo wachimbaji wadogo na kati, wafanyabiashara wa madini, watoa huduma migodini, wataalamu kutoka taasisi za Wizara ikiwemo Shirika la Madini la Tanzania (STAMICO) pamoja na taasisi za kifedha wako ziarani nchini China kwa lengo la kubadilishana uzoefu katika Sekta ya Madini baina ya Tanzania na China.
No comments