WENYE PhD WAKARIBISHWA VETA
Dar es salaam - Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Anthony Kasore, amewakaribisha Watanzania kushiriki kilele cha maadhimisho ya miaka 30 ya VETA, yatakayofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam kuanzia Machi 18 hadi Machi 21, 2025, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).
Akizungumza katika kipindi cha Jambo Tanzania cha kituo cha runinga cha TBC1, Machi 17, 2025, Kasore amesema maadhimisho haya ni fursa kwa Watanzania wa rika zote kujifunza kuhusu elimu ya ufundi stadi na nafasi zake katika maendeleo ya taifa.
"Tunawakaribisha wananchi wote, kuanzia waliomaliza darasa la saba hadi wenye Shahada ya Uzamivu (PhD), kwani hata waliomaliza shahada wanaweza kujiunga na VETA," amesema Kasore, akisisitiza kuwa wamewahi kuwa na mwanafunzi mwenye PhD aliyesomea uchomeleaji.
Maadhimisho hayo yataangazia mambo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mifumo ya ufundishaji, uzoefu wa wahitimu wa VETA na manufaa yao, pamoja na ushiriki wa waajiri ambao wataeleza sifa na ujuzi wanaoutarajia kutoka kwa waajiriwa. Pia, kutakuwa na midahalo kuhusu maendeleo ya elimu ya ufundi na jinsi serikali inavyoendelea kuimarisha sekta hiyo.
Kasore ameongeza kuwa serikali imefanya maboresho makubwa katika sekta ya elimu ya ufundi, hatua ambayo inatekeleza dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuifanya elimu ijikite katika ujuzi.
"Sera mpya ya elimu inahimiza elimu ya ujuzi, ndiyo maana sasa tunazungumzia elimu ya amali, na mabadiliko haya yatasaidia kuzalisha Mtanzania mwenye ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi," amesisitiza Kasore.
VETA imeendelea kuboresha miundombinu na kuongeza wigo wa upatikanaji wa elimu ya ufundi ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata ujuzi unaowawezesha kujiajiri au kuajirika katika sekta mbalimbali.
Post Comment
No comments