Breaking News

WAKULIMA 2500 WA VITUNGUU WANUFAIKA NA RUZUKU YA MBOLEA KARATU, SERIKALI YAPONGEZWA

Wakulima 2500 wa vitunguu wilayani Karatu wamenufaika na mpango wa mbolea za ruzuku tangu kuanza kwake mwezi Agosti 2022 mpaka Januari 2023.

Mpango huo umesaidia sana  kupunguza gharama za uzalishaji wa zao hilo kufuatia kiasi cha mifuko 12 kutumika kwa heka moja ya vitunguu. 

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Karia Magaro alipokuwa akizungumza na wanahabari kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) waliofika ofisini kwake kufuatilia manufaa yaliyotokana na mpango wa ruzuku kwa mwaka wa fedha, 2022/2023.

"Suala la ruzuku za mbolea limepokelewa kwa furaha sana na wakulima na limekuja kwa wakati.

Nimpongeze sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kuwajali sana wakulima na waziri wa kilimo, Hussein Bashe kwa kuratibu Mfumo wa mbolea za ruzuku" Magaro alisema .

Amesema, wakulima 13622  wamesajiliwa katika mfumo wa mbolea  ya ruzuku kati ya  wakulima 15,000 waliopo katika halmashauri yake na kueleza waliosalia ni wale wanaohisi hawahitaji kutumia mbolea japo juhudi za kutoa elimu zinaendelea ili wajue umuhimu wa kutumia mbolea katika kuongeza uzalishaji na tija.

Aidha, Mkurugenzi Magaro alibainisha kuwa, mahitaji ya mbolea kwa wakulima wa eneo la Mang'ola ni la  muda wote kutokana na wakulima kujihusisha na kilimo cha umwagiliaji hivyo hulima mara tatu kwa mwaka.

Ameongeza kuwa, vitunguu ni zao linaloiingizia halmashauri  zaidi ya nusu ya mapato ya ndani  na  kueleza kwa mwaka 2021/2022 kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kimepatikana kufuatia ushuru wa zao la kitunguu.  

Mkurugenzi Magaro amemaliza kwa kuiomba serikali kuendelea kutoa ruzukuya mbolea na kueleza  hiyo itakuwa faraja sana kwa wakulima.

Kwa upande wake, mkulima wa kitunguu, mahindi maharage na mbogamboga Mustapha  Mbwambo amesema amepata nafuu sana ya uzalishaji wa vitunguu baada yaruzuku ya mbolea kuanza kutolewa naye kufanikiwa kununua mwezi Septemba 2022.

Amesema, walipoanza msimu mwezi Juni 2022 gharama ya mbolea ilipanda sana na ilipanda ghafla na hivyo kuwawia ugumu kwenye shughuli za kilimo.

Amesema, heka moja ya kitunguu inahitaji mifuko 12 ya mbolea hivyo kupunguziwa kwa zaidi ya nusu ya bei ya mbolea kumewapunguzia gharama za uzalishaji na hivyo kuwawezesha kuongeza maeneo ya kilimo yanayowahakikishia kuongezeka kwa uzalishaji na tija kwenye kilimo.

Ameishukuru serikali kwa kuwajali na kuamua kuwapa ruzuku na kuomba mpango huo uendelee kwani unawasaidia kupunguza gharama za pembejeo walizokuwa wakizipata.

No comments