NSSF YAZINDUA VUKA KIDIJITALI DARAJA LA NYERERE
Ni mfumo unaowezesha watumiaji wa vyombo vya moto kujisajili na kulipa mara gharama za vuka, sasa mtumiaji anaweza kulipia kifurushi cha siku, wiki au mwezi
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umetekeleza kwa vitendo maagizo yaliyotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita ya kupunguza gharama ili kuwaondolea kero wananchi na watumiaji wa Daraja la Nyerere, Kigamboni, Dar es Salaam.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mfuko kuzindua rasmi mfumo wa NSSF ‘Bridge Portal’ ambao unawezesha mteja kununua bando la siku, wiki au mwezi ili kupita na chombo cha moto katika Daraja la Nyerere.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi wa mfumo huo leo Februari 21, 2023, Mkurugenzi wa TEHAMA wa NSSF, Donald Mhaiki, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na NSSF ulipitia gharama za tozo za darajani kwa vyombo vya moto vinavyopita katika daraja hilo na kufanya punguzo kubwa la tozo.
Mhaiki amesema punguzo hilo lilianza kutumika rasmi mwezi Mei mwaka 2022, ambapo Mfuko ulikuja na punguzo zaidi kwa kuanzisha mfumo wa bando ambapo mtumiaji wa daraja anaweza kupita kwa kulipia kwa siku, wiki au mwezi.
Amesema kabla ya kuanza kwa mfumo huu, mtumiaji wa daraja alikuwa anatumia wastani wa shilingi 90,000 kwa mwezi, lakini kwa kutumia mfumo huu hivi sasa mtumiaji wa daraja anatumia shilingi 35,000 kwa mwezi.
Mhaiki amesema Mfumo huu unamuwezesha mtumiaji kusajili chombo chake cha moto na kwa chombo ambacho hakijawahi kupita, mteja anatakiwa afike ofisi za NSSF zilizopo Darajani kwa ajili ya kusajili na hatimaye kununua bando. Amesema chombo ambacho kimeshawahi kupita darajani angalau mara moja, mteja anaweza kusajili kupitia mfumo wa kielektroniki bila kulazimika kufika ofisi za NSSF.
Naye, Emmanuel Masika ambaye ni msimamizi wa Daraja la Nyerere, amesema mfumo huu wa bando umerahisisha upitaji wa darajani kwa maana ya kuondoa foleni na upitaji wake ni rahisi.
Meneja wa NSSF Mkoa wa Kigamboni, Judith Kebara, amesema huduma hiyo ni mzuri na ni fursa kwa wanachama na Watanzania kwa ujumla.
No comments