Breaking News

DKT. BITEKO AZINDUA KAMATI MPYA YA TEITI

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amezindua Kamati ya tano ya Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji  katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) inayosimamia  viwango vya uwazi na uwajibikaji kwa lengo la kuboresha mapato na manufaa yatokanayo na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini.

Dkt. Biteko amezindua Kamati hiyo leo 9 Februari, 2023 katika ukumbi wa Abdulkarim Mruma uliopo jijini Dodoma itakayofanya kazi  kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2023 mpaka 2026.

Sambamba na uzinduzi huo, Dkt. Biteko amewakabidhi wajumbe wakamati hiyo vitendea kazi vitakavyo tumika katika kutekeleza majukumu yao ambavyo ni Sheria ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia na Kanuni zake, Sheria ya Madini , Sheria ya Petrol, Sheria ya Usimamizi wa Mafuta na Gesi pamoja na EITI Standard 2019.

Akizungumza juu ya majukumu ya kamati hiyo, Dkt. Biteko amesema kuwa, katika kutekeleza majukumu hayo wajumbe wa kamati hiyo wanatakiwa kufanya  tafiti mbalimbali ambazo zitawezesha kuchangia ukuaji wa sekta ya Uziduaji hapa nchini kwa kuzingatia taarifa za malipo na mapato za wachimbaji wadogo wa madini zinawekwa wazi na kulinganishwa.

Akielezea  juu ya madini mkakati  Dkt. Biteko amesisitiza kuwa kwa sasa dunia  inasisitiza utafutaji na uchimbaji endelevu unaozingatia utunzaji wa mazingira  hivyo ameitaka kamati kuisimamia Taasisi hiyo katika tafiti mbalimbali zitakazowezesha serikali na wadau wa maendele kuwekeza katika madini hayo muhimu duniani.

Akifafanua kuhusu mhamo wa nishati, ameitaka kamati kuweka nguvu  katika kuhamasisha  uwazi na kutoa elimu  kuhusu mhamo wa nishati kwa kushirikiana  na taasisi zingine za Serikali katika kuandaa mpango wa kutambua madini mkakati na kuishauri Serikali juu ya maendeleo endelevu ya sekta ya Uziduaji nchini.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kamati ya TEITI Ludovick Utouh amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye  utajiri mkubwa wa rasilimali zinazosimamiwa na TEITI ambayo ilijiunga na Asasi ya EITI Mwezi Februari 2009 ili kuhakikisha kuwa inaweka mifumo ya Uwazi na Uwajibikaji  katika usimamizi wa Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia kwa lengo la kuboresha  mapato na manufaa yanayotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini.

Sambamba na malengo hayo, Utouh amefafanua kuwa, TEITI itaendelea  kuboresha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo nchini kwa lengo la kufikia kiwango cha mchango wa asilimia 10 katika la Pato la Taifa ifikapo 2025 kulingana na Mpango wa Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano.

Uzinduzi wa kamati ya tano ya TEITI umeudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Danstan Kitandula, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Msafiri Mbibo.



No comments