CUF YAMTAKA ALIYEKUWA DPP JAJI BISWALO KUJIUZURU KUPISHA UCHUNGUZI WA SAKATA LA UPOTEVU WA MABILIONI YA FEDHA OFISI YA DPP
Chama cha Wananchi (CUF) kimemtaka aliyekuwa mwendesha mashtaka wa serikali (DPP) Jaji Biswalo Maganga kuachia ngazi hili kupisha uchunguzi wa tume iliyoundwa na rais Samia Hassan kuchunguza nini kilitokea na kupelekea sehemu ya fedha za umma kutojulikana zilikowekwa.
Akizungumza makao makuu ya chama cha hicho buguruni jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema tume hiyo haitoweza kufanikiwa kutekeleza majukumu yake kwa uhuru kutokana na aliyekuwa Mkurugenzi wa Ofisi hiyo kipindi cha "Plea Bargaining" bado anashikilia nafasi ya juu katika moja ya ofisi ya utoaji haki, yaani Mahakama Kuu.
"Chama cha wananchi CUF kinamtaka aliyekuwa Mkurugenzi wa Mashtaka hata wale watumishi waliokuwa wakimsaidia kipindi hicho cha “Plea Bargaining” wasimamishwe kazi kupisha uchunguzi wa Tume huru hili uchunguzi wake uwe wenye tija na kufuata Utawala wa Sheria pamoja na kurejesha imani ya Watanzania katika ofisi husika" Alisema Prof Lipumba.
Alisema hatua ya Mheshimiwa Rais kubadilisha Mkurugenzi wa ofisi hii peke yake haikutotosha kumaliza mizizi iliyopelekea kujitokeza kwa mapungufu haya ya kiofisi, hivyo ili kuhakikisha ofisi hizi zinabadilika kabisa na kutekeleza majukumu yake kwa Muktadha wa Misingi ya Kikatiba, Demokrasia, Haki sawa kwa wote na Utawala bora kwa mujibu wa sheria watuhumiwa wote wasamishwe kazi kupisha uchunguzi.
Aidha Prof. Lipumba aliongeza kuwa Tume hoyo pia ichunguze na kubainisha kama kuna viongozi na taasisi nyingine zilizohusika katika sakata hili pamoja na kuchunguza fedha taslimu zilizopokelewa na zilizowekwa kwenye akaunti za benki.
"CUF tunaitaka Tume ichunguze na kubainisha kama kuna viongozi na taasisi nyingine zilizohusika katika sakata hili pamoja na kuchunguza fedha taslimu zlizopokelewa na kuwekwa akaunti pamoja na mali zisizohamishika zilizowekwa kama dhamana kwa wale walioshindwa kulipa fedha taslimu, kama bado ziko mikononi mwa Serikali au zimerejeshwa kinyemela" Alisema na kuongeza kuwa
"Chama cha wananchi CUF kina imani kuwa Tume itafanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, bila woga wala upendeleo na tunaitakia utekelezaji mwema wa majukumu yake na wale watakaobainika wamehusika katika sakata hili ama la upotevu wa fedha au matumizi mabaya ya ofisi husika basi wachukuliwe hatua za kisheria ili kuzuia matukio kama haya kujirudia tena".
No comments