Breaking News

TIC YASAJILI MIRADI 132 KATIKA KIPINDI CHA MWEZI JULAI HADI NOVEMBER 2022.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kimesema jumla  ya miradi 132 yenye thamani ya zaidi Dolla bilioni 3.16 ambayo imetoa ajira 21,297, imesajiliwa kwa kipindi cha Julai mwaka huu hadi Novemba mwaka huu.

Aidha,TIC imesema miradi hiyo ni ongezeko la asilimia 22.2 ikilinganishwa na miradi 108 iliyosajiliwa katika kipindi kama hiyo mwaka jana huko kwa upande ajira imeongezeka kwa asilimia 57 kutoka ajira 13,578 mwaka jana hadi ajira 21,297 mwaka huu.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi  Mkuu (TIC), John Mnali, wakati akizungumza na waandishi wa habari akitoa taarifa ya miradi iliyosajiliwa katika kipindi cha Julai hadi Novemba mwaka huu. 

Aidha, Mnali ametaja miradi iliyosajiliwa mwaka huu ni sekta ya viwanda  67, Sekta ya usafirishaji miradi 25, utalii miradi 12, kilimo 9, huduma 8, majengo ya Biashara 7, Rasilimali watu 3 na Sekta ya fedha 1. 

Kadhalika, Mnali, amesema katika miradi hiyo 132 iliyosajiliwa miradi  50 inamilikiwa na wageni, wakati miradi 30 inamilikiwa na watanzania huku miradi 52 inamilikiwa kwa ubia kati ya Watanzania na wageni.

Hata hivyo, Mnali amesema kuongezeka kwa miradi hiyo kumechangiwa na jitihada za serikali za kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizoko nchini kupitia ziara mbalimbali za viongozi wa kitaifa nje ya nchi na juhudi za serikali katika kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.

No comments