Wafanyabiashara na Wawekezaji Kutoka CZECH Wavutiwa na Mazingira ya Uwekezaji Nchini
Naibu waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, mhe. Miloslav Stasek amewasili nchini akiwa ameambatana na baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini humo ikiwa ni ziara ya kuangalia fursa za uwekezaji hapa nchini Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es salaam katika mkutano na waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC ), Dkt Maduhu Kazi amesemba ujumbe huo umekuja ikiwa ni jitihada zilizofanywa na balozi wa Tanzania Nchini Ujerumani Dr. Abdalah Possi ambaye amekua akishawishi makampuni makubwa kuja kuwekeza hapa nchini.
Dkt. Kazi alisema wawekezaji na wafanyabiashara hao wameonesha nia ya kuwekeza katika sekta ya kilimo hasa Pamba, Viwanda vya nguo pamoja na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo,
"Leo tumepokea ujumbe kutoka Jamhuri ya Czech, tumezungumza mambo mengi tunaamini tutafanya vizuri katika uwekezaji na biashara, TIC baada ya kufanya taratibu zote tunaamini tutapata wawekezaji wazuri na wenye manufaa makubwa kwa nchi yetu" Alisema Dkt. Kazi.
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech, mhe Miloslav Stasek alisema mazungumzo yao na TIC yamekuwa ya mafanikio makubwa yeye pamoja na wajumbe alioongozana nao wamejadiliana na uongozi wa TIC na kupata fursa ya kutambua masuala mbalimbali ya kuongeza ushirikiano ili kuimarisha sekta ya uwekezaji kati ya Czech na Tanzania kwa maslahi ya pande zote mbili.
"Tanzania ina fursa nyingi za uchumi, hivyo tumekuja kuangalia mazingira ya uwekezaji tutashirikiana vyema na serikali kupitia Wizara ya Biashara na Viwanda katika kuhakikisha makampuni yetu makubwa yanakuja kuwekeza". Alisema Mhe.Stasek.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa tunatangaza fursa za biashara na uwekezaji.
“Serikali imejikita zaidi katika kutangaza Fursa za kupata wafanyabiashara kutoka Czech zinazidi kuongezeka hapa nchini, hivyo nitoe rai kwa sekta binafsi kuchangamkia fursa za biashara na uwekezaji,”
Dkt. Abdalah Possi aliongeza kuwa huu ni wakati wa wafanyabiashara wa Kitanzania kuchangamkia fursa ya kuingia ubia na makampuni ya kigeni katika kufanya biashara na kuwekeza kwenye sekta mbalimbali kukuza sekta ya viwanda na uchumi wa nchi.
No comments