Jamhuri ya CZECH Yakabidhi Vitanda Viwili Vya Kisasa Vya Wagonjwa Ocean Road
Jamhuri ya Czech kwa kushirikiana na kampuni ya Linet Group pamoja na Gama Pharmaceuticals (T) Limited imefanikiwa kuchangia vitanda viwili vya kisasa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road vyenye thamani ya shilingi milioni 16 za kitanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek amekabidhi vitanda hivyo kwa taasisi hiyo na kupokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dr. Julius Mwaiselage pamoja na viongozi wengine wa taasisi mbalimbali za Serikali.
Mhe. Staŝek amesema Serikali ya Czech itaendelea kushirikiana na Tanzania kwa karibu katika kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia uliopo baina ya mataifa hayo mawili.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dkt. Abdallah Possi ameishukuru Czech kwa ushirikiano ambao imekuwa ikiutoa kwa Tanzania na kuahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano wake na Czech kwa maslahi ya pande zote mbili.
Awali akitoa salamu za shukrani, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dr. Julius Mwaiselage ameishukuru Jamhuri ya Czech kwa msaada huo na kuongeza kuwa pamoja na msaada huo, bado taasisi hiyo ina kabiliwa na changamoto ya uhitaji wa vitanda vya kisasa 25 ambapo hadi sasa wanavyo vitanda nane (8) tu hivyo kuwa na uhitaji wa vitanda vingine 17.
Meza kuu wakifuatilia hafla fupi ya makabidhiano ya vitanda viwili vya kisasa vilivyotolewa na Jamhuri ya Czech kwa kushirikiana na kampuni ya Linet Group pamoja na Gama Pharmaceuticals (T) Limited.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Czech Mhe. Miloslav Staŝek pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road Dr. Julius Mwaiselage wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi na wawakilishi wa Taasisi mbalimbali mara baada ya kukabidhi vitanda viwili vya kisasa Ocean Road.
No comments