Machinga Waomba Kukutana na Rais Samia
Shirikisho la Umoja wa Machinga Tanzania (Shiuma) limemuomba Rais Samia Suluhu Hassan akutane nao kumweleze kero walizonazo ili ajue namna ya kuzifanyia kazi.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Oktoba 20, 2021 na Makamu Mwenyekiti wa wamachinga Taifa, Steven Lusinde wakati akitoa ufafanuzi kuhusu vurugu za wamachinga zilizotokea jana katika soko la Kariakoo.
Lusinde alisema Samia ndiye Rais wa kwanza kutenga fungu la fedha kwa ajili ya maendeleo ya wamachinga na kwamba mkutano huo utamwezesha kupokea maoni kutoka kwao moja kwa moja nini Sh5 bilioni zifanye kwa manufaa ya wajariamali hao wadogo.
“Tunamshkuru sana Rais ametoa zaidi ya Sh5 bilioni kuhakikisha yanaorodheshwa maeneo hayo kwa ajili ya wamachinga, sisi tupo pamoja na yeye akutane na sisi wamachinga wa mikoa yote tumueleze hata asiyoyajua.
“Yeye mwenyewe apange wapi ili tumweleze changamoto zetu na tushauri fedha hizo zinaweza kutatua changamoto zipi mengi yasiweze kutokea, tunashkuru suala hili amekasimisha kwa wakuu wa wilaya, mikoa na wakurugenzi hivyo utekelezaji umewezekana,” amesema Lusinde.
Amesisitiza kuwa viongozi wanatakiwa wawashirikishe machinga maeneo wanayotaka kwenda kuwaweka ili kuondoa sintofahamu.
“Watushirikishe sisi changamoto zipo, ukiangalia maeneo mengi waliyoenda bila usumbufu walitushirikisha tunaamini kila kitu kitaenda sawasawa,” amesema Lusinde.
Source Mwananchi
No comments