Filamu 120 Zafuzu Mchujo wa Awali Kuwania Tuzo za Filamu 2021
Serikali kupitia Bodi ya Filamu Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu imeandaa Tuzo za Filamu Tanzania 2021 (Tanzania Film Festival Awards 2021 - TAFFA) ili kutambua mchango wa tasnia ya sanaa ikiwemo filamu ambapo kilele chake ni Disemba 4, 2021.
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dodoma Oktoba 20, 2021 Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo amesema Serikali kupitia Wizara ya Sanaa, Utamaduni Michezo tangu Septemba 11, 2021 ilizindua rasmi tamasha la tuzo hizo Jijini Dar es Salaam na kufuatiwa na zoezi la ukusanyaji wa filamu kutoka mikoa 8 tofauti, ambayo ni Mtwara, Morogoro, Tanga, Mbeya, Arusha, Dodoma, Mwanza na Dar es Salaam.
Amesema filamu zaidi ya 600 zilipatikana kutoka katika mikoa hiyo, ambapo timu ya wataalam ilichambua filamu hizo kwa kuzingatia vigezo mbalimbali, ikiwemo ubora wa sauti, ubora wa mwanga, ubora wa picha, mwendelezo wa matukio kati ya tukio moja na lingine, matumizi ya lugha, uhariri, kanuni ya nyuzi 180, pamoja na mwaka wa utayarishaji filamu ambao ni 2019 hadi 2021.
Ameongeza kuwa kupitia vigezo hivyo, filamu zaidi ya 120 zimepita katika mchujo wa awali kutoka katika makundi mbalimbali yakiwemo tamthilia, filamu ndefu, filamu fupi, animesheni, pamoja na makala.
“Baada ya mchujo huu wa kwanza, zoezi linalofuata ni kuzionesha filamu hizo, likifuatiwa na zoezi la wananchi kupiga kura kwa baadhi ya vipengele na vingine kupitiwa na waamuzi (judges) kwa ajili ya kupata washindi. Filamu hizi zote zitaanza kuoneshwa kupitia chaneli ya Sinema Zetu, katika kisimbuzi cha Azam” amefafanua Dkt. Kiagho
Amewasihi wadau mbalimbali kuendelea kupata taarifa zaidi kuhusu tuzo hizo kupitia kurasa rasmi za mitandao ya kijamii, ikiwemo Instagram (@tanzania_film_board), Facebook (Bodi ya Filamu Tanzania) na tovuti ya Bodi www.filmboard.go.tz).
No comments