Breaking News

TAKUKURU Temeke Yapokea Jumla ya Malalamiko 78 Na Kuyapatia Ufumbuzi.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Temeke imesema itaendelea kuongeza kasi katika kufanya chambuzi za mifumo katika maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa juu ya utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo ikiwemo sekta ya Elimu, Afya na Uchukuzi ili kuongeza ufanisi katika maeneo hayo. 

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati akitoa taarifa ya utendaji kwa kipindi cha  miezi mitatu kuanzia Julai 1 mpaka Septemba 30 Mwaka huu, Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Temeke, Bw. Donasian Kessy  amesema katika kipindi hicho wamepokea Jumla ya malalamiko 78. 

Alisema baadhi ya malalamilo ambayo yameripotiwa katika kipindi hicho ni pamoja na 18 yamehusiana na rushwa ambapo kati yake 15 watoa taarifa wame elimishwa na kushauriwa na matatu yalihamishiwa katika idara nyingine.

"Katika kipindi hicho tumepokea Malalamiko 60 yanayohusu Rushwa, malalamiko 43 uchunguzi unaendelea, malalamiko matatu uchunguzi wake umekamilika na malalamiko 14 majalada yake yamefungwa" alisema Kessy

Aidha bw. Kessy aliongeza  kuwa katika kipindi cha Oktoba mpaka Disemba  mwaka huu wamejipanga kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo ili kuziba mianya hasa katika ujenzi wa miradi ya maendeleo ambapo serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi.

"Mapambano dhidi ya rushwa ni ya kila mwana Temeke hivyo ili kuufanya mkoa wa Temeke kuwa sehemu nzuri ya kuishi isiyokuwa na rushwa ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki kikamilifu katika mapambano haya". Alisema bw. Kessy.

Alisema Takukuru mkoa wa Temeke katika kuhakikisha wanafanikiwa kutokomeza vitendo vya rushwa wataendelea kushirikiana na Chama cha Skauti Tanzania kutoa elimu ya Rushwa kwa vijana wenzao ili kujenga dunia iliyo bora.

No comments