Breaking News

Baba Halisi Wa Uzao Afanya Maombi Kumwinua Rais SAMIA Na Wasaidizi Wake, Pamoja Kuwabariki Waandishi Katika Ibada Maalumu

Baba Halisi wa Uzao amefanya maombi maalum na kuwabariki Waandishi zaidi ya 50 kutoka vyombo mbalimbali vya habari walio hudhuria Ibada Maalum ya Kuwabariki Waandishi wa habari, iliyoandaliwa na Kanisa Halisi la Mungu Baba na kufanyika Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegeta Jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuwabariki Waandishi hao kutoka vyombo mbalimbali vya Habari, Baba Halisi alifanya shukrani (maombi) Maalum ya kumuinua Rais Samia Suluhu Hasaan na Wasaidizi wake; Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa na viongozi wengine wote wa Serikali na Jamii kwa jumla.
"Maovu yote hutokana na Mamlaka, hivyo tunawainua (kuwaombea) viongozi wote wa Taifa letu ili Mungu Baba awalinde na kila ovu, wabarikiwe na kuwa huru katika utendaji wao, wafanye kazi zao kwa bidii na maarifa ili Tanzania iendelee kuwa na amani na utulivu na kuinuka zaidi kiuchumi na Kijamii", alisema Baba Halisi katika Ibada hiyo Maalum.
Katika kuwabariki, Baba Halisi wa Uzao aliwaita Waandishi wa habari hao kusimama katika eneo Maalum mbele yake, baada ya kufika wakiwa kwenye sura za furaha alianza kuwafanyia maombi (shukrani) aliyosema kuanzia baada ya Ibada hiyo watakuwa wamepata Baraka za Mungu Baba ikiwemo kutochukiwa tena na jamii kwa ajili ya kazi zao na kufanya kazi zao za uandishi zikiwemo za kijamii, Biashara, siasa na Burudani kwa weledi na bila kubagua.
Maombi hayo Baba Halisi wa uzao aliyahitimisha kwa kuwanywesha kila mmoja 'Damu safi' (Maji yaliyo barikiwa) na kisha kuagana nao kwa kuamuru Makuhani wa Kanisa hilo kuwapatia soda waandishi hao na wote walioshiriki kwenye Ibada hiyo Maalum wanywe kabla ya kuondoka.
"Nimefurahi sana kuwaona hawa wanangu (waandishi), basi Makuhani wapatieni soda wote, na Uzao wote waliomo humu wanywe soda, tufurahie sherehe hii kubwa", akasema Baba Halisi wa Uzao kabla ya kufunga rasmi Ibada hiyo Maalum.





 

No comments