Breaking News

TUZO ZA FILAMU 2021 ZITAKUWA ZA UWAZI NA HAKI

Hayo yalisemwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Kiagho Kilonzo Tarehe 26 Septemba, 2021, alipokuwa akijibu hoja za Wadau wa Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini katika Kikao Kazi na Wadau hao kilichofanyika Jijini Dar es Salaam.

“Serikali kupitia Taasisi ya Bodi ya Filamu, imeanzisha Tuzo za Filamu kwa mara ya kwanza ijulikanayo kama Tanzania Film Festival Awards 2021, "Tuzo hizi ni za Serikali kwa asilimia 100, hivyo zitasimamia misingi ya uwazi na haki kwa kila Mshiriki kwasababu Serikali ni ya kila mmoja na haina sababu ya kudhurumu haki ya watu wake” alisema Dkt. Kiagho.

Akiendelea kuelezea, Katibu Mtendaji huyo alisema kuwa, lengo la kuanzisha Tuzo hizo ni kutambua mchango wa Wanatasnia ya Filamu katika utendaji wa kazi zao, pamoja na kuhamasisha utengenezaji wa Filamu bora kupitia uwekezaji unaoendelea kufanyika katika Tasnia hiyo.  Kaulimbiu ya Tuzo hizo ni FILAMU NI BIASHARA, lengo likiwa ni kubadilisha mtazamo wa Filamu za Kitanzania kibiashara katika Masoko ya ndani na nje ya nchi.

Dkt. Kilonzo aliwaeleza Wadau wa Filamu waliohudhuria katika kikao hicho kuwa, wanajukumu la kuzipokea Tuzo hizo kwasababu ni zao na zina lengo la kuinua Tasnia ya Filamu nchini pamoja na mapungufu au changamoto zozote zitakazo jitokeza.

"Hatutakiwi kuzilaani Tuzo hizi, tutakapozilaani hazitadumu na zitakufa, kama kuna lolote ambalo haliko sawa ni jukumu letu sote kulijadili na kulirekebisha ili kufanikisha Tuzo hizi zitakazokuwa na manufaa kwa Tasnia yetu". Alisema Dkt. Kilonzo.

Kwa upande wake Raisi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Bw. Eliya Mjatta alisema kuwa, Shirikisho la Filamu limekuwa likishirikiana na Serikali katika mchakato wa Tuzo hizo tangu mwanzo hadi sasa, na wataendelea kushirikiana katika kuhakikisha  kunakuwa na mafanikio.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Tanzania (TDFAA) Bw. Salum Mchoma almaarufu Chiki Mchoma, aliipongeza Serikali kupitia Bodi ya Filamu kwa kuanzisha Tuzo hizo kwa kuwa Tasnia ya Filamu inahitaji  ushindani hivyo kupitia Tuzo ushindani utaongezeka miongoni mwa Wanatasnia wa Filamu na kuleta mabadiliko katika Soko la Filamu zetu.


No comments